Wednesday, January 9, 2013

SURUA na IMANI POTOFU vilinisababishia ULEMAVU: EDWARD JUMA MWITA

0 comments


Naitwa Edaward Juma Mwita, mkazi wa Musoma mjini mkoa wa Mara. 

Nina ulemavu wa macho (uoni) ambao sikuzaliwa nao ila tu niliugua surua nikiwa na miaka mitatu (3). Baada yakupelekwa hospitalini ikagundulika kua macho yangu yalikua yameharibika na nisingeweza kuona tena. Tatizo langu lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na imani potofu zilizokua zimetawala kwa kipindi hicho. Baada ya kuugua surua ilisemekana kua huyu mtoto (mimi) hatakiwi kuonekana kwa watu hivyo niliwekwa ndani. Badae mama ndo alikuja kugundua kua macho yalikua yanaharibika baada ya kufungua kope za macho yangu, badae wakaamua kunipeleka hospitalini lakini walikua wameisha chelewa.
Nilibahatika kusoma mpaka elimu ya sekondari lakini sikufanikiwa kuendelea zaidi kwasababu ya gharama za masomo pamoja na ukosekanaji wa vifaa. Kwasasa naishi na mama yangu sijaoa wala sina mchumba.
Changamoto kubwa ninayo kumbananayo ni upatikanaji wa mahitaji muhimu ya kuniwezesha kuishi kama mwanaadamu wa kawaida, kwamfano; chakula, malazi na mavazi inakua vigumu sana kuvipata hasa pale unapokua huna shughuli ya kukupatia kipato.
Wakati mwingine sio rahisi sana kukubalika katika jamii. Inachukua muda mrefu kwa jamii kuja kukukubali, labda waone tu umefanya kitu flani ambacho kinawezakua ni kivutio kwao. Kwamfano; Niliwahi kumwelekeza jamaa mmoja aliyekua anatafuta duka flani hapa Musoma, nikamwambia kua twende mimi ntakupeleka lakini hakutaka kuniamini. Sasa hii ni sehemu ya changamoto ninazo kumbananazo sababu kile ambacho mi nakitenda hakiataaminika mpaka mwenye macho akithibitishe kwamba ni kweli nakiweza ama sikiwezi. Kwahyo kukubalika kwangu kutategemea uwezo wangu katika kukiweza hicho kitu. Hii inapelekea mambo mengi kua magumu kufanyika sababu sio kitu kizuri kumwambia mtu kua hiki kitu ntakufanyia halafu asiwe na imani!.
Changamoto nyingine iko katika swala la fimbo nyeupe ambazo ni chache. Pamoja na kua chache bado hazitoi ishara kukufahamisha kama kuna kitu flani mbele yako ambacho unatakiwa kua tayari kukikabiri, hii inapelekea ugumu flani katika kutembea kwa watu wasio ona. Kama kungekua na uwezekano basi tungeweza kupatiwa fimbo zenye uwezo huo ili tuweze kutembea salama na kwa uhakika.
Nilikua na ndoto zakuja kua mwanasheria au mwalimu lakini sijafanikiwa kuzifikia ndoto zangu. Pamoja na kusoma kwa changamoto nyingi sana hasa katika elimu ya msingi ambapo ilikua inakulazimu kuwategemea watu wakusomee ili uweze kuandika lakini bado nilikua na ndoto za kuendelea na nilifanya hivo. Nilianza kupata shida kubwa sana kipindi nilipoingia sekondari, ilikua inamlazimu mtu awe na pesa ili amtafute mtu umpatie fedha ili akusomee na wewe uandike. Kwasababu kinachofanyika sekondari baada ya mwalimu kufundisha na kuandika notisi huwezi kusomewa humohumo darsani kama ilivokua shule ya msingi. Inakubidi baada ya vipindi umtafute mtu mwenye macho kwa muda wako na pesa yako mwenyewe ukaenae kwenye chumba maalumu akusomee na uanze kuandika masomo ya siku nzima. Pamoja na hayo, karatasi (kwaajili ya kuandikia watu wenye ulemavu wa macho) zinakua ni duni maana upatikanaji wake ni tatizo, kunawakati zinaweza kukosekana mpaka kipindi cha mwezi mzima na kwakipindi hicho chote walimu wanaendelea kufundisha na notisi zinaongezeka pia. Kwahyo utakapoanza tena kuandika masomo tisa utakua umepoteza muda mwingi sana kiasi kwamba hata muda wakujisomea unakua hadimu pia.Hivyo inakupatia mzigo mkubwa tena wa kukisoma kitu ambacho kilisha fundishwa muda mrefu uliopita na wakati huohuo kukisoma kitu kilichofundishwa kwa wakati huo. Hali hii inasababisha walemavu hasa wasioona warudi kua ombaomba katika mitaa mbalimbali ya nchi hii.
Naiomba jamii iweze kuwathamini na kuwasaidia watu wenye ulemavu kwasababu watu wenye ulemavu hususani wasioona wanaishi katika mazingira magumu sana. Asiyeona asipokua na pato lolote anapata taabu sana. Naiomba jamii iwe tayari kuwasaidia watu wenye ulemavu, nafahamu kua kuna wenzetu ambao sio waaminifu lakini kama hao watu wakikutokea na ukafahamu mwachie Mungu tu kwakua wewe umeishatoa. Pia naiomba jamii ishiriki kikamilifu katika kuwasaidia watu ambao wako katika mazingira yanayoweza kuwapelekea kua walemavu ilikusudi waepukane na hali hii ya ulemavu kwani ni tatizo kubwa mno.
Watu wenyeulemavu wenzangu nawashauri tuendelee kujitahidi pale tunapokua tumepata nafasi mbalimbali kama shule au ajira ili tuweze kujiendeleza. Pia kile ambacho tunakipata kama misaada  inatakiwa tukitumie kwa uaminifu mkubwa ili mtu anapokuja tena kuangalia kile unachokifanya akute umefanya vizuri. Kwahyo nivyema tukafanya kazi kulingana na uwezo aliotuwezesha Mungu, tusilemae tu kwa kisingizio cha ulemavu.
Naziomba asasi mbalimbali hasa zile zinazojishughulisha na maswala ya watu wenye ulemavu zifanye kazi zake kulingana na lengo la kuanzishwa kwake, wasitumie vibaya misaada wanayopewa. Pia wajitahidi kuvumbua vitu mbalimbali vinavoweza kuwasaidia watu wenye ulemavu sio tu kuendelea kutoa habari kuhusu haki zetu.
Serikali yetu ijitahidi sana kutekeleza wajibu wake. Tunazo rasilimali nyingi sana ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuwasaidia watu wenye ulemavu. Hivyo rasilimali zilenge makundi yote. Misaada itolewe kwa vyama vya watu wenye ulemavu ilikusudi hata watu wenye ulemavu waweze kukopa kupitia vyama vyao wenyewe. Pia vilevile katika zile nafasi kumi (10) za wabunge wa kuteuliwa zingetolewa nafasi kwaajili wa vyama vya watu wenye ulemavu kuteuliwa ili tuweze kupata wawakilishi katika vyombo vya kufanya maamuzi.
 Nawaomba sana ndugu zangu wasioona ambao wako mashuleni wajitahidi sana kusome kwabidii pamoja na changamoto nyingi wanazokumbana nazo.
Read More ->>
 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |