Monday, February 25, 2013

Kulemaa viungo hakuzuii akili kufanya kazi: YOHANA MAGAYI

5 comments


YOHANA MAGAYI
Naishi katika wilaya ya Bunda mkoa wa Mara, nina mke na watoto.

Kazi yangu ni ufundi seremala fani niliyoipata katika chuo cha walemavu Yombo Dar es salaam mwaka 1985  - 1986 na pia Milongo Mwanza 1988 – 1989. Pamoja na hayo nilipata mafunzo ya utetezi wa haki za binaadamu kwa watu wenye ulemavu kutoka ICD, kwahyo mimi ni mwanaharakati pia.
Kwa mujibu wa maelezo ya wazazi wangu, nililemaa baada yakuwa nimeanza kutembea nikiwa na umri wa miaka miwili (2). Niliugua polio iliyonipelekea kukaa kwa muda mrefu na baadae kunisababishia ulemavu kwa ujumla.
Nilipata changamoto kubwa katika kuliendea swala zima la kuoa, hata yule niliyekua natarajia kumuoa kabla alishtuka kusikia kua mimi mlemavu nataka kumuoa! Alifikiri kua tutazaa watoto wenye ulemavu pia. Baada ya mimi kupata mtoto wa kwanza mwaka 1988, aliniandikia barua kwamba sasa niko tayari kuolewa na wewe kwakua sikutegemea kama ungekuja kuzaa watoto wazima. Namshukuru sana mke wangu wa sasa kwa uvumilivu tangu 1988 mpaka leo.
Swala la kuoa au kuolewa nichangamoto sana kwa watu wenye ulemavu wapo wengi wanaotamani kupata wenzi wao lakini inashindikana sababu ya ulemavu walionao. Wengine wanapata wenzi lakini jamii zao zinaendelea kulalamika kwa kuona mtu asiyekua mlemavu akiolewa na mlemavu.
Kuna vikwazo vingi katika kupambana na maisha, kwa ujumla mimi ni Mwenyekiti wa kijiji na niligombea na watu wazima wenye viungo vyao vyote, jamii ilinielewa na kunichagua kuwaongoza. Lakini bado napambana na vikwazo vingi kwasababu kuna watu wanajitokeza na kuuliza maswali: ‘Hivi watu wa jamii hii hawana akili kabisa, inawezekanaje watu zaidi ya 5000 mkakubali kuongozwa na mlemavu, hamuoni kwamba huu ni udhaifu mkubwa?’. Wakati mwingine swala la kupata kipato kwa mtu mwenye ulemavu imekua ni changamoto sana. Kwa mfano sisi tunaoishi katika mkoa wa Mara ambapo shughulikubwa ya kipato ni kilimo, kitu ambacho kwa udhaifu wetu hatuwezi. Shughuli ya pili ni Uvuvi ambayo pia ni ngumu kwetu, kwahyo unakuta kupata kipato ni ngumu sana. Nashukuru kwa kazi yangu hii ya Useremala japokua ni ngumu lakini natenda na ninapata mahitaji. Nayashukuru pia mashirika haya ya ICD na mashirika mengine ambayo tunapokutana yanatupa changamoto za namna ya kujitegemea kuliko kutegemea misaada.
Mwanzoni kabisa nilikua na fikra ya ufundi toka mwanzo na ilikua ya jadi kwasababu hata baba zangu walikua wachongaji. Baadae baada ya kuingia shule nilitamani sana kua mhasibu, lakini ndoto hiyo haikufika baada ya kukosa mtu wakuniendeleza katika masomo pamoja na uwezo mkubwa niliokuanao darasani. Kwakweli mzee wangu alipata udhaifu wa kifikra, aligoma kabisa na kusema kwamba wewe hata nikikusomesha hutoweza kwenda kokote. Namlaumu sana kaka yangu ambaye alikua Dar es salaam wakati huo. Nilimwomba anitafutie nafasi ya kurudia mitihani lakini hakuweza kutekeleza hilo. Nilipokwenda Yombo nilitegemea ningepata nafasi ya kusomea uhasibu lakini baada ya kuikosa nikaamua kujiingiza kwenye ufundi kama ndoto yangu ya kwanza ilivokua. Nashukuru kwamba leo hii inanisaidia sana kwakweli. Imenitunza na kunipa mafanikio makubwa, mpaka sasa nina watoto saba (7) na watatu kati yao wamefikia elimu ya sekondari na ninasomesha wengine hakuna mtoto ambaye amenishinda. Nimefikia malengo yangu kwakweli maana namtunza mke wangu nawatunza watoto wangu pia na sijawahi kumpa mtu kunilelea mtoto hata mmoja kati ya hao saba wote.
Naishukuru sana jamii ya kijiji ninamo ishi, mpaka kufikia kunipa hadhi yakuwa mwenyekiti wa kijiji ni jambo la kushukuru sana kwakweli, inamtizamo wa pekee kabisa, kitu ambacho hata Rais hana mtizamo huo. Naishauri jamii kwa ujumla kuwaamini na kuwaheshimu watu wenye ulemavu, kilicholemaa ni baadhi ya viuongo tu, kitu kinachofanya kazi kumudu maisha ya mtu hasa ni akili, kwahyo tunaweza tukiwezeshwa. Jamii itambue kwamba sisi ni moja kati ya jamii inayofanana nao.
Naishauri serikali kupunguza ule udumavu ilionao. Kwa mfano; kuna sheria ya watu wenye ulemavu lakini wameidumaza tu tangu ilipo pitishwa mwaka 2010 mpaka leo haijatungiwa kanuni. Mpaka tunaelekea katika katiba mpya bado sheria ile haifanyi kazi na bado sina imani kama itafanyakazi. Naishauri serikali ihakikishe sheria ile inapata kanuni na kufanya kazi. Pia walemavu wapatiwe nafasi za kujiendeleza. Nashauri pia serikali ivifungue na kuviendeleza vyuo vya watu wenye ulemavu. Kwa mfano chuo cha Milongo Mwanza kimefungwa kasababu ya kukosa walimu wakati serikali ina bajeti.
Nayashauri mashirika yasiyokua ya kiserikali kama ICD, CCBRTna mengine mengi kuongeza juhudi sababu ndio yaliyosababisha watu wenye ulemavu kutambua haki zao. Nayashauri yaendelee kupiga kelele kwakuwa ndiyo yaliyotupatia mwanga, kwakuwa serikali imeweka kabatini sheria na taratibu zote za kumpatia mtu mwenye ulemavu huduma na haki zake.
Read More ->>
 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |