Monday, January 28, 2013

‘Tukitaka kuibadili jamii yetu na kuifanya jumuishi ni lazima tuangalie ni vitu gani ambavyo sio jumuishi kwanza.’ JONAS LUBAGO

0 comments


JONAS LUBAGO
Kwa jina naitwa Jonas Lubago, natoka chama cha wasioona Tanzania  (TLB). Ninaishi Dar es salaam ambapo nina mke mmoja na mtoto mmoja kwa sasa. Nimeajiriwa na naendeleza shughuli zinazo husu maswala ya watu wenye ulemavu za kila siku.

Ulemavu nilionao ni ulemavu wa uoni (macho). Historia yangu ya ulemavu siifahamu vizuri, ila kwa harakaharaka imeonekana ni tatizo la kuzaliwa nalo ambalo limekua likiendelea kujidhihirisha kadri umri unavoenda. Nilianza kusoma kwenye shule za kawaida na kujifunza kama watoto wengine. Nilipofika darasa la tatu ndo walimu wakagundua kua sioni sawasawa. Nilihamishiwa katikati ya darasa lakini sikuweza kuona, nikawekwa mbele ya darasa lakini tatizo likabaki vilevile. Kuanzia wakati huo ndo nikaanza kujifunza maandishi ya nukta nundu ambayo niliendelea kuyatumia katika ngazi zote za kielimu mpaka kwenye hatua ya masters. Nina masters ya ualimu (MA Education).
Katika maisha ndoto zinabadilika kutokana na ngazi uliopo kwa wakati huo. Mimi sikuwaza kua nani au kushika nafasi gani, lakini mara zote tangu nikiwa mdogo ninafikiria jinsi ninavyoweza kua kwenye nafasi inayoweza kunipa fursa ya kuwahudumia watu wenye ulemavu na jamii kwa ujumla. Niwe sehemu ambayo ikitokea changamoto yoyote inayo wahusu watu wenye ulemavu na inahitaji kufanyiwa maamuzi, basi changamoto hiyo itatuliwe kwa kutoa kauli au neno tu. Hiyo ndo nafasi ninayo tamani kuwa nayo siku moja. Siwezi kusema nataka niwe waziri kwasababu tunaona mawaziri wengi ambao wanashindwa kufanya maamuzi, pengine tunakosa mtu anayeweza kufanya maamuzi ambayo athari zake zitaonekana kwenye maisha ya mtu mmojammoja.
Kwa taifa letu kuna mambo ambayo tumeishapiga hatua, vitu kama sera, na sheria ziko nyingi sana. Kwahyo mi naona upande wa policy work tumeisha fanya vyakutosha, lakini hizi sera na sheria zote zinazowekwa kama hazifanyi impact kwenye maisha ya mtu mmojammoja (individuals), bado hizi sera zinakua hazina maana sana. Ndomaana nasema natamani niwe kwenye sehemu ambayo ntasema sera flani haijatekezwa, wewe halimashauri flani, wizara flani, au taasisi flani fanya hiki na tukaona impact kwa watu wenye ulemavu na maisha yao kubadilika.
Katika kuliendea swala la kupata mwenza (mke) sikukumbana na changamoto kwakweli. Nadhani hii ilitokana na aina ya shule nilizo zoma, mimi nimesoma intergrated schools tokea shule ya msingi. Hili lilinipa fursa ya kuzijua skills za kukaa na watu mbalimbali tangu nikiwa mdogo. Nilijifunza namna ya kuchangamana na kuishi na wengine, pia ni mbinu gani unaweza kuzitumia katika kumpata mwenza. Naweza nikasema nilikua na advantage tu, kwamba nilikua na choice nyingi za kuchangua. Tatizo linakuja kwa jamii inayo waangalia! Watu wanaanza kujiuliza maswali, hivi huyu alimwonaje huyu mwenzake kwamba ni mzuri? Mkienda sehemu kama kutembea watu wanawaangalia sana, na yeye akiona hivo anaanza kujiuliza mbona watu wananiangalia sana? Kwahiyo changamoto tulizonazo zinatoka upade wa jamii na sio upande wake yeye au jinsi anavo nielewa au namna nilivompata.
Katika maisha kuna changamoto nyingi, zipo zile za kitaasisi ambapo unakuta tasisi nyingi sana sio rafiki. Lakini nikivua miwani na kujiangalia mimi mwenyewe na kuangalia jamii ya watu wenye ulemavu naona changamoto nyingi sana.
Kuna mifumo mingi ambayo haiwafikishii mawasiliano watu wenye ulemavu na hivyo kuwanyima haki ya taarifa. Yako maendeleo mengi ambayo hayawalengi watu wenye ulemavu, kwahiyo wanakua nje ya mfumo wa maendeleo yanayo ilenga jamii. Kuna uwezeshwaji ambao hauwafikii watu wenye ulemavu. Kwahiyo ukija kuhesabu mfumo mmojammoja uliopo ndani ya jamii, utaona kwamba watu wenye ulemavu hawajalengwa moja kwa moja. Kitu hiki kinawafanya wawe nje ya uwanda mpana wa maendeleo ya jamii. Na ndiomaana utaona watu wenye ulemavu wengi ni maskini, hawana elimu, wanaishi maisha ya utegemezi na wengine wakifika sehemu watu wanawashangaa, hii ni kwasababu ya mifumo na changamoto zilizopo.
Tukitaka kuibadili jamii yetu na kuifanya jumuishi ni lazima tuangalie ni vitu gani ambavyo sio jumuishi kwanza. Kwamfano, upande wa maamuzi sio jumuishi, jamii zina mitazamo ambayo sio jumuishi. Kwahyo kwenye jamii panatakiwa pawekewe mitazamo jumuishi. Mzazi akipata mtoto mwenye ulemavu kitu chakwanza kujiuliza itakua, mimi nimepata mtoto ambaye ni tofauti na wengine, kwahiyo jamii itanionaje ama? Hilo nalo ni shida. Ukja kwenye mifumo inayofuata kama elimu utagundua kua ni baguzi kabisa. Kwasababu hauweki mazingira ya kumuingiza mtoto mwenye ulemavu kwenye mfumo ambao unatumiwa na watoto wengine. Kwahiyo weka mfumo wa elimu ambao ni jumuishi. Mfumo wa elimu jumuishi usichukuliwe kama wimbo; uwe mfumo ambao mtu mwenye ulemavu wa kawaida mfano, ulemavu wa viungo, alibino, na kadhalika ataweza kusoma kwenye shule za kawaida. Na kwa ulemavu mwingine ambao ni mkubwa kidogo kuwe na shule kama nilizosoma mimi (intergrated schools) shule mchanganyiko. Kwahiyo unawezakua na mifumo miwili ambayo itaongeza nguvu kwenye swala la elimu.
Ukija kwenye mfumo wa utoaji maamuzi je tunapata uwakilishi? Hapo ndo nafikia hatua yakusema kua hata mfumo wa uchaguzi tunaoutumia hapa nchini, ni mfumo mbaya. Yaani yule aliyepata kura nyingi kupita wenzake, hata kama ameongoza kwa kura moja, huyo ndo atachukuliwa kama kiongozi wenu. Hata kama mlikua watu 100 na wakwanza akapata kura 35, hawa waliobaki wakagawana kura chini ya 35 inamaana utakuta huyu mwenye 35 anawaongoza watu wengine 35 ambao hawakumchagua. Sasa tungekua na mfumo wa uwiano katika uchaguzi (propotional representation) utakao mruhusu yoyote aliyejaribu kufanya maamuzi, hayapotei katika ngazi ya kwanza, bali yatakwenda yanakusanywa mpaka ngazi ya taifa. Mwishowe utakuta kile alichokifanya kwenye ngazi ya chini kabisa kinakua na athari mpaka kwenye ngazi ya taifa. Kwahiyo nasema hata mfumo wa uchaguzi sio jumuishi na unahitajika mfumo ambao una wiano.
Nivigumu sana kuilaumu jamii kwa lolote linalotokea kwasababu ni tamaduni ambazo tumezaliwa nazo, kinachotakiwa ni uhamasishwaji katika nyanja zote. Kwasasahivi mabadiliko yanaonekana sio kama zamani,  zamani tulikua tunauawa baada ya kuzaliwa, lakini kutokana na maendeleo yaliyopo na kuwafanya watu wajifungulie hospitali inakua vigumu kuuawa tena.
Watu wenye ulemavu wanatakiwa kujiamini, watu kama sisi ambao tumebahatika kupata elimu ndo tunatakiwa kua vioo. Hii itaipelekea jamii kutuona na kuanza kutuamini. Kimsingi tunaacha athari katika jamii, unapoenda sehemu na kutoa elimu kwa wazazi na jamii na ikagundulika kua na wewe ni mlemavu inawapelekea hata wale wazazi walio waficha watoto wao ndani kuamua kuwatoa na kuwapeleka shule.
Taasisi mbalimbali zinatakiwa zijiwekee taratibu za namna ya kuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Kwa kiwango kikubwa naona serikali imeishafanya mambo mengi kwa watu wenye ulemavu, kuna sera, sheria na miongozo mbalimbali. Tatizo lililopo serikalini nikwamba hakuna mawasiliano kati ya ngazi ya serikali kuu na halimashauri. Kama sera hizi na mipango iliyoko kwenye ngazi ya kitaifa zingewekewa mpango wa kuwaelimisha wafanya maamuzi kwenye ngazi ya halimashauri tungepiga hatua. Kwahiyo serikali iweke mpango wakuwaelimisha taratibu watu wa halimashauri ili waweke maswala ya watu wenye ulemavu katika mipango yao ya kila mwaka.
Read More ->>
 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |