Sunday, April 14, 2013

UBINAFSI WAMKERA MGOSI CHACHA

4 comments


Naitwa Mgosi Chacha, naishi Musoma mjini katika mtaa wa mkendo. Nina ulemavu wa viungo, kwasasa sijafanikiwa kuwa na familia bado natafuta maisha.

Nilizaliwa nikiwa mzima kama watu wengine, ila baada ya kufikisha umri wa miaka miwili nilipatwa na maradhi ya kienyeji, ambayo kimira yalikua kama miiko kwetu. Baba alikutana na vitu flani ambavyo ni miiko kimira, kwahiyo mi nilipozaliwa ndo nikapatwa na hayo maradhi. Baba na mama walikosa ushirikiano katika swala zima la kuniuguza mimi, hii ilimpelekea mama kunihudumia jinsi anavojua mwenyewe hatimaye ndo nikapata ulemavu.
Changamoto kubwa ninayo kumbananayo ni ubinafsi uliojikita katika jamii. Kwamfano mtu kama mimi nina elimu ya ufundi (welder) na nimesoma chuo kabisa, lakini nikifika ofisini kwa mtu kuomba kazi sipewi kazi. Nakataliwa na kutimuliwa katika mazingira yao, pamoja na kuwaonesha vyeti vyangu kama uthibitisho wa uwezo wangu katika kuifanya kazi hiyo. Nikutokana na hali ya ulemavu nilionao jamii hunichukulia kama mtu asiyeweza kufanya kazi. Na hii ndo ilinipelekea kuamua kujiajiri na kufanya kazi ya kushona viatu.
Naishauri jamii kutuangalia sana sisi watu wenye ulemavu na wasitutenge sababu kulemaa viungo sio kulemaa kila kitu cha mwili wako. Jamii ijitahidi kuwa karibu sana na sisi kwasababu sisi ni kama wao na wao nikama sisi.
Nawashauri watu wenye ulemavu kuondoa ile kasumba ya kutokutaka kujitegemea kwasababu ya ulemavu walionao. Mlemavu anawezakuwa na familia na akategemewa kama watu wengine. Mlemavu sio mtu wa kutegemewa kusaidiwa kwa kila kitu, inabidi kujisaidia wakati mwingine. Ukiwa umelemaa viungo tu na unaakili ya kukuongoza katika mambo mengine kwanini usijitegemee?
Naona kwa wakati huu serikali imeanza kutupa matumaini ya kutukumbuka, hapo awali tulikuwa tumesahaulika kabisa. Nashauri serikali kuziboresha ofisi zake ili ziweze kufikika na watu wa aina zote pasipo kuwabagua watu wenye ulemavu (hususani walemavu wa viungo). Hii itatuondolea ile adha ya kuwaagiza watu wakatuzungumzie haja zetu na badala yake tutaweza kujieleza wenyewe.
Mashirika ya watu binafsi kidogo wana uelewa, hata wakiamua kufanya kitu wanakifanya kwa kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali. Nayashauri mashirika na taasisi mbalimbali kushiriki katika kuhakikisha walemavu mbalimbali (ambao wengi wao hawana elimu) wanapatiwa haki zao za msingi.
Read More ->>
 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |