Friday, March 15, 2013

“Mwanamke kuolewa na mtu mwenye ulemavu huonekana kama ‘Msimbe’ katika jamii inayo nizunguka.” KIGOMBE MAGIGE KIGOMBE

1 commentsNaitwa Kigombe Magige ni mwenyekiti wa watu wenye ulemavu wilaya ya Bunda, naishi katika kijiji cha Manyamanyama Bunda. Nina mke na watoto wanne (4), elimu yangu ni elimu ya sekondari niliyo hitimu mwaka 1993 katika shule ya sekondari Ikizu. Kwahivi sasa nashughilika na shughuli za kushona viatu pamoja na shughuli nyingine ndogondogo za kujikimu kimaisha.
Mimi ni mlemavu wa viungo, ulemavu huu niliupata nikiwa na miaka mitatu (3) nadhani ilikua ni polio kwasababu mzazi wangu alinambia kua niliugua homa kali ghafla, badae wakaenda kunichoma sindano baada ya kurudi mguu wa kulia ukawa unakataa kufanya kazi. Walijaribu kuwa wanachimba shimo na kunisimamisha ndani kwa siku nzima lakini hamna nafuu, matokeo yake miguu yote ikapooza na nikaishia kuwa hivi.
Nilikutana na changamoto mbalimbali katika swala la kuoa, mke wakwanza niliyemwoa nilikaanae baada ya siku watu wakaanza kumcheke na kumwambia wewe utaakaje na mtu mwenye ulemavu? Baada ya muda baba mkwe na mama mkwe wakaamua kunisaliti na kumwondoa kwangu na akachukuliwa na bwana mwingine ambaye mpaka sasa wanajificha. Baadae nilipata mke mwingine na kumwoa, kidogo yupo lakini changamoto haziishi, anasema wanamcheka na kumwambia wewe nikama ‘Msimbe’ sababu mme wako mwenyewe ni kilema sijui ulimpendea nini? Changamoto kama hizo hazikosi maana katika jamii sio wote wanaoelewa kuwa ulemavu ni mapenzi yake Mungu, leo unaweza kuwa mzima baadae ukawa mlemavu. Wengine wanaona ulemavu kama ni balaa katika jamii, kwakweli tuna kumbana na changamoto kubwa katika jamii pamoja na serikali, tunanyanyaswa kwakweli.
Manyanyaso yanakuja kwasababu ukienda serikalini hata kuomba namna ya kuwezeshwa ili uweze kuboresha kazi zako serikali wanakwambia hawana fedha. Ukienda katika benki wanakwambia una nini cha kuweza kujidhamini ili tukupe fedha? Ukienda kwenye asasi hizi zinazotoa mikopo wanasema mlemavu!? Huyu anataka achukue fedha ale apotelee kwasababu hana aseti inayoweza kumdhamini aweze kukopa. Sasa mara nyingi watu wenye ulemavu tumekua ombaomba kutokana na kukosa mitaji yakuweza kujiajiri sisi wenyewe, pia serikali haitupi ajira wala kupanga mafungu kwaajili ya watu wenye ulemavu, tumekua ni watu tuliosahaulika, tunaongelewa katika magazeti na redio lakini kivitendo hatumo kabisa.
Ndoto zangu nyingi sijazifikia, nilikuwa na makusudi kwamba ntakapo kuwa mtumzima niwe na familia, nipate maisha ya kujitegemea niwe na nyumba niwe na biashara zangu nzuri zakufanya. Watoto nimeishapata na mke ninae, tatizo linakuja kwenye ajira na biashara zangu (hasahasa kujiajiri mi mwenyewe). Sijapata mtaji wakutosha wakunifanya nijiajiri mwenyewe, sijaweza kuajiriwa na mtu, kwa hali hiyo bado naishi kwenye nyumba duni ya kupanga. Ukilinganisha gharama za maisha ya kupanga, unakuta chumba wanataka elfu ishirini (20000), sasa sisi watu wenye ulemavu tunapoenda kutafuta nyumba za kupanga kwa mtu, unakuta huyo mtu anaanza kuwa na wasiwasi kama mlemavu anaweza kulipa kodi, mwingine atataka akupe banda tu uishi kwasababu anaweza kukuvumilia uishi bure kwenye banda kwasababu hawezi kukuweka kwenye nyumba nzuri ambayo anawezakuitumia kupata fedha. Hali hii imekua ni ngumu kwangu mpaka sasa inanipa mawazo sana.
Nawashauri wenzangu watu wenye ulemavu wasife moyo, wawe na juhudi za kutafuta fedha na maisha wajitolee kujitumikisha ili waondokane na unyanyapaa huu tunaoupata. Pia watu wenye ulemavu tusijishushe sana kuwa hatuwezi kitu, tuwe na nia na imani kua tunaweza iwapo tukiwezeshwa, tusifike mahala kutegemea kwamba tuwe ombaomba. Wale ambao tunaujuzi tujitahidi kuutumia ujuzi wetu katika kujisaidia, tusiendelee kuwa mitaani na vibakuli tukiombaomba matokeo yake tunatukanwa tunanyanyaswa na kukerwa na jamii. Nawale wanaoenda shule wajitahidi kusoma kwa bidii kwasababu swala la ulemavu sio kitu cha ajabu ni maumbile tu yanayotokana na mapenzi ya Mungu.
Jamii ione tatizo la ulemavu ni la watu wote na jamii kwa ujumla,ione mlemavu kama mtu anayestaili upendo na kusaidiwa ili aweze kujimudu kimaisha. Jamii ione ninamna gani inaweza kumsaidia mtu mwenye ulemavu kua na maisha bora ili ajione kama watu wengine. Jamii ichukulie ulemavu kama si laana au dhambi, iuone ulemavu kama mapenzi ya Mungu. Isiwanyanyase wala kuwatenga, kwamfano unakuta kwenye familia nyingine walemavu wanafungiwa ndani na kufichwa hawataki waonekane, wanaonakwamba wewe ni kitu cha ajabu. Inawezekana mtu akawa anatembea mzima lakini akawa mlemavu kuliko huyo mklemavu anayetengwa.
Asasi na taasisi zinazojishughulisha na maswala ya watu wenye ulemavu zifanye utafiti na kuwasaidia kikweli watu wenye ulemavu, isiwe kuwatumia watuwenye ulemavu kama chambo cha kupatia fedha na kutumia wenyewe hiki sio kitu kizuri. Kama ni asasi imeamua kuwasaidia watu wenye ulemavu iwasaidie kwa juhudi zote, iwapatie nyenzo za kutembelea, iwape mikopo ya kuwawezesha kujishughulisha na uzalishaji mali, isichukulie kwamba mlemavu ni mtu wa kulishwa tu. Asasi nyingi zinawachukua watu wenye ulemavu na kuwakusanya pamoja kwa kuwapatia mahitaji ambayo sio ya kimaendeleo na hapo wanakua wamewanyanyasa watu wenye ulemavu badala ya kuwasaidia kwasababu hawawaoneshi picha halisi ya maisha yakuweza kujitegemea.
Serikali imekua na danganya toto, maranyingi imekua ikisema kuwa inategema mafungu kwaajili ya watu wenye ulemavu lakini haifanyi hivyo kihalisia. Ukija kwenye sheria ya mwaka 2010 ya watu wenye ulemavu, hiyo sheria imetungwa lakini hakuna mlemavu anayejua hiyo sheria inasema nini? Imebaki tu kwenye makaburasha yao. Serikali hiyohiyo inasema inawawakilishi wa watu wenye ulemavu bungeni, lakini wawakilishi hao wanatoka maofisini na kwenye vyama vya siasa na kwenda kwenye bunge! Hawajatoka kwenye bunge na kuja kukaa na watu wenye ulemavu na kujua walemavu wanataka nini, wanashida gani? Na kero hizo zikapelekwa bungeni, imekua watu hawa wanatetea maslahi ya vyama vya siasa na watu walio wateua. Kwahyo tunafikiri kwamba serikali haijatenda haki kwa watu wenye ulemavu kuwapa uwakilishi.  Serikali ilisaini mkataba wa haki za binaadamu kwa watu wenye ulemavu, lakini imekua kama danganya toto, katika mkataba huo unaonesha wazi kwamba hata baiskeli inatakiwa inastahili serikali isaidie watu wenye ulemavu lakini cha ajabu serikali haifanyi hivo badala yake wanaziachia asasi. Sisi sio wa asasi sisi ni watanzania na serikali inawajibika kwa watu wote, hakuna mafungu.
Rais naye anaonekana kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu kwasababu; hakuna mlemavu anayeteuliwa kua mkuu wa wilaya, waziri, wala mkuu wa mkoa wote unakuta ni watu wenginewengine tu! Hivi mlemavu hawezi kweli? Hivi hakuna walemavu wenye elimu? Wapo niwengi ila kilichopo nikwamba tumetengwa kwavile wanasema walemavu wengi hawakusoma. Tunaendelea kunyanyaswa na kupuuzwa hata kiongozi wa serikali anazidi kuonesha unyanyapaa huo.
Napenda pia kuzungumzia swala la wenzetu walemavu wa ngozi, hawa niwatu wakawaida kama watu wengine lakini jamii imewachukulia kama ni ‘deal’, biashara na kuwafanya waishi bila amani, wasiwasi, na hofu kubwa kutokana na rangi waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Swala la serikali kusema iwakusanye na kuwaweka pamoja, pia ni sawa na kuwanyanyapaa. Tunaomba serikali itoe elimu kwa jamii kuwa watu wenye ulemavu nisawa na watu wengine. Nakama mtu akibainika kuwa ameua mtu mwenye ulemavu wa ngozi, naomba serikali ingeweka amri au sheria kali ya kuwanyonga watu wa aina hiyo.
Read More ->>
 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |