Monday, December 10, 2012

HAYA NDO YAKWETU

0 comments


RISALA YA SHIVYAWATA, VYAMA VYAKE, NA VYAMA VYA HUDUMA KWA WATU WENYE ULEMAVU KWA MGENI RASMI, WAZIRI
MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA MIZENGO KAYANZA PETER PINDA KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA WATU WENYE ULEMAVU DUNIANI LEO TAREHE 3 DESEMBA 2012 – MARA MUSOMA.


Mheshimiwa Mgeni Rasmi- Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mh. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii 
Mh. Kamishna – Idara ya Ustawi wa Jamii,
Mh. Mkuu wa Mkoa wa Mara;
Weheshimwa Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi na viongozi wengine wote wa Serikali kwa vyadhifa zenu
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania
Waheshimiwa wadau wa Masuala ya Watu Wenye Ulemavu
Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Musoma na Dar es Salaam
Waheshimiwa viongozi wa vyama vya siasa,
Waandishi wa Habari ,
Ndugu wageni waalikwa; Mabibi na mabwana itifaki imezingatiwa.

Awali ya yote napenda kutumia nafasi hii kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii muhimu kwa watu wenye ulemavu Duniani.

Aidha, tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwako Mgeni Rasmi kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi katika kuadhimisha siku hii muhimu ya watu wenye ulemavu nchini na duniani kwa kote.

Tunafahamu kuwa una majukumu mengi ya Kitaifa na Kimataifa, kukubali kwako mwaliko wetu ni uthibitisho wa wazi kwa Watanzania, kuwa wewe ni mtu wa watu na unayewajali Watanzania bila kujali tofauti zao. 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya watu wenye ulemavu wote hapa nchini tumekuwa tunaadhimisha siku hii kila mwaka tangu kutolewa tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa katika Azimio No. 47/3 la 1992. Lengo la maadhimisho haya ni kuhamasisha jamii, serikali pamoja na wadau katika sekta mbalimbali kutambua uwezo na mchango wa watu wenye ulemavu, Ikiwa ni pamoja mchangamoto zinazowakabili ili kujenga mazingira yanayotoa fursa sawa katika ushiriki wao kwenye shughuli za maendeleo katika Nyanja mbalimbali za jamii.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, mwaka huu 2012 ambao ni mwaka wa ishirini wa maadhimisho haya hapa nchini umebebwa na kauli Mbiu ONDOSHA VIKWAZO ILI KUJENGA JAMII JUMUISHI INAYOFIKIKA KWA WOTE”


Mheshimiwa Mgeni Rasmi, katika maadhimisho haya tunapenda jamii itambue vikwazo anavyokabiliana navyo mtu mwenye ulemavu, ili ishiriki kwa dhati katika kuviondoa na kumwezesha mtu mwenye ulemavu ashiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuzifikia huduma zote za kijamii.

Mheshimiwa mgeni rasmi, katika safari ndefu ya kudai huduma rafiki kwa watu wenye ulemavu kutambuliwa, kuthaminiwa pamoja na kuheshimu utu wa mtu mwenye ulemavu, tunapenda kuishukuru sana serikali kwa yafuatayo:-

-          Kuandaa sera ya Maendeleo ya watu wenye ulemavu ya 2004
-          Kutambuliwa kwa watu wenye ulemavu katika MKUKUTA
-          Kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya watu wenye ulemavu wanaopata elimu kuanzia shule ya msingi hadi Elimu ya Juu
-          Kusaini na kuridhi Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za watu wenye ulemavu wa 2006.
-          Kupitisha sheria Na.9 ya haki za watu wenye ya 2010
-          Kuwezesha watu wenye ulemavu angalau kushiriki na kuadhimisha siku za watu wenye ulemavu kupitia Bajeti za Halmashauri
-          Kusambazwa kwa waraka wa serikali kote nchini kupitia TAMISEMI unaoelekeza utekelezaji wa utoaji wa matibabu bure kwa watu wenye ulemavu katika hospitali zote za umma na kuzuia kufukuzwa watoto wenye ulemavu pindi wanapokosa ada kuanzia July, 2012.
-          Kuendelea kupata ondoleo la kodi kwa vifaa vya watu wenye ulemavu vinavyoingizwa nchini kama msaada kwa matumizi ya watanzania wasio na uwezo wa kununua vifaa hivi ambavyo ni aghali sana kwa mtu mwenye kipato cha chini.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Pamoja na masuala yote tuliyoeleza hapo juu, bado kuna changamoto kadhaa zinazotukabili watu wenye Ulemavu ambazo imekuwa vikwazo kwa watu wenye ulemavu kufikia huduma za jamii pamoja na kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo hizi ni pamoja na:-
-          Upatikanaji wa taarifa muhimu katika mifumo isiyorafiki kwa watu wenye ulemavu. Viziwi wamekuwa wakikosa taarifa muhimu zinazotangazwa kupitia Luninga kutokana na kutokuwepo wakalimani wa lugha ya alama. Hivyo kuwafanya wakose kufuatilia taarifa muhimu kama Hotuba za Rais kila mwezi, mijadala ya kielimu, taarifa za habari na vipindi vya Bunge
-          Miundo mbinu isiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu, majengo mengi yanayotoa huduma kwa umma hayafikiki na watu wenye ulemavu hii ikiwemo ofisi inayoratibu masuala ya watu wenye ulemavu.
-          Kukosekana kwa alama maalumu za barabarani ambazo zingewawezesha madereva na watu wengine kuziheshimu ili watu wenye ulemavu kumudu kutumia barabara kwa uhuru. Vile vile vyombo vya usafiri kama mabasi, traini na vyombo vya majini pamoja na viwanja vyote vya ndege si rafiki kwa watu wenye ulemavu kwa kukosa nyenzo muhimu na nafasi maalumu kwa watu wenye ulemavu wanapotumia vyombo hivi.
-          Ruzuku ndogo kwa vyama vya watu wenye ulemavu isiyokidhi mahitaji ya msingi katika kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu na isiyotolewa kwa wakati, na miaka mingine kupita bila kupatiwa.
-          Kukosekana kwa uwakilishi wa watu wenye ulemavu katika vyombo vingi vya maamuzi kuanzia ngazi za serikali za mitaa hadi serikali kuu, hii ni kwa vile si wote katika vyombo hivi wenye ujuzi juu ya mahitaji halisi ya watu wenye ulemavu, hivyo kupelekea mipango mingi ya maendeleo kutokuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.
-          Kukosekana kwa ofisi ya kudumu kwa Shirikisho la Vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania ambalo limekuwa kiunganishi baina ya vyama vya watu wenye ulemavu, taasisi zinazohudumia watu wenye ulemavu, Serikali na wadau mbalimbali

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,  kutokana na changamoto  tulizozibainisha hapo juu, SHIVYAWATA na wadau wa masuala ya watu wenye ulemavu tunapendekeza yafuatayo kwa Serikali na kupitia kwako Mgeni Rasmi,

-          Katika kukabili kikwazo cha upatikanaji wa habari, Serikali ihimize uwepo wa wakalimani wa lugha ya alama katika vyombo vya habari kila inapotolewa taarifa muhimu kwa umma. Na kwa kuanzia walau iwezeshe uwepo wa Wakalimani katika Television ya Taifa, vikao vyote vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Hotuba za Mh. Rais za kila mwezi kwaajili ya viziwi kupata habari. Pia iwezeshe uchapaji wa nyaraka muhimu kama sera, sheria na mipango mikakati ya serikali na miongozo mbali mbali ya kazi kwa maandishi ya nukta nundu na maandishi yaliyokuzwa ili kutoa fursa kwa wasioona na wale wenye uoni hafifu kuweza kuzifahamu na kuzitumia ipasavyo .
-          Tunaiomba Serikali kupitia SUMATRA ihakikishe vyombo vyote vya usafiri kwa umma kama vile mabasi, daladala, treini na meli vinavyoagizwa vinakidhi viwango vya ufikikaji kwa watu wenye ulemavu.
-          Tunaiomba Serikali ihakikishe kuwa ujenzi wa viwanya vya ndege, majengo ya umma chini ya NSSF, NHC, TBA na mamlaka nyingine pamoja na barabara unaoendelea hapa nchini hususani kwenye miji, miundo mbinu yake ikidhi viwango vya ufikikaji kwa watu wote wenye ulemavu.
-          Serikali iwezeshe vyuo vya Mafunzo kwa watu wenye ulemavu vilivyo chini ya Idara ya ustawi wa jamii ambavyo vimefungwa kufufuliwa, ili kuwapa ujuzi watu wenye ulemavu waweze kuishi maisha ya kujitegemea
-          Serikali, izielekeze na kuziwezesha Mamlaka za Elimu na Ufundi (VETA), SIDO na Chuo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,  kufanya utafiti na kuanza kutengeneza vifaa vya kujimudu kwa watu wenye ulemavu kama fimbo nyeupe, baiskeli na pikipiki za miguu mitatu hapa nchini ili kukabili ughali wa nyenzo hizo muhimu kwa wenye ulemavu.
-          Serikali ikamilishe Uchapaji wa Kanuni za sheria ya watu wenye ulemavu kama ambavyo imeahadi mara kadhaa ili kuwezesha utekelezaji wa sheria ya watu wenye ulemavu ya 2010
-          Serikali ikamilishe uundwaji wa Baraza la watu wenye ulemavu ili kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa Sheria ya watu wenye ulemavu iliyoanza kufanya kazi rasmi 2010.
-          Serikali iwezeshe upatikanaji wa Ofisi ya kudumu ya Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA) ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea pindi wafadhili wa nje watakapositisha ufadhili wa pango la Ofisi (katika hili tunapenda kukumbushia ahadi yako iliyoitoa 2008 tulipokutembela nyumbani kwako Dodoma) bado tungali tunasubiria.

Ndugu Mgeni rasmi, kwa mara nyingine tunaomba Serikali iafiki kuhamishia uratibu wa maswala ya watu wenye Ulemavu katika Wizara yenye mamlaka juu ya Wizara nyingine, kama vile Ofisi ya Waziri Mkuu au Ofisi ya Rais. Hiki kilio chetu kinatokana na kwamba Idara inayoratibu kwa sasa haiwezi kuagiza wizara nyingine kujumuisha na kutekeleza upatikanaji wa mahitaji ya watu wenye ulemavu katika mipango yao. Katika hili bado tunakumbuka nia yako ya dhati ya kutekeleza hili japo hatujui lilikwama wapi.

Ndugu Mgeni Rasmi, SHIVYAWATA na wadau wote haki za watu wenye ulemavu tunatambua na kuthamini azma ya serikali kuanzisha na kusimamia mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya ya nchi baada ya miaka 50 ya uhuru. Fursa hii ni muhimu katika kuhakikisha kuwa jamii inazingatia haki na usawa miongoni mwa makundi yote hapa nchini. Hivyo tunaiomba serikali ihakikishe kuwa sauti za watu wenye ulemavu kuhusu haki na mahitaji yao yanazingatiwa kikamilifu katika katiba mpya ijayo. Watu wenye ulemavu tunaamini kuwa vikwazo vitapata ufumbuzi tu endapo katiba ya nchi itatambua bayana haki na mahitaji yatu.

Mwisho Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tunaomba kutumia nafasi hii kuwashukuru marafiki na wadau wa masuala ya watu wenye ulemavu ambao wamechangia kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha maadhimisho haya. Aidha, tunapenda kukushukuru tena wewe binafsi Mh. Mgeni Rasmi na wageni waalikwa wote kwa kujumuika nasi leo tukiamini kuwa serikali itasikia kilio cha watu wenye ulemavu.

Ahsante

…………………….
Lupi Maswanya
Mwenyekiti-SHIVYAWATA   
Read More ->>
 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |