Naitwa Edaward Juma Mwita, mkazi wa Musoma
mjini mkoa wa Mara.
Nina ulemavu wa macho (uoni) ambao sikuzaliwa nao ila tu
niliugua surua nikiwa na miaka mitatu (3). Baada yakupelekwa hospitalini
ikagundulika kua macho yangu yalikua yameharibika na nisingeweza kuona tena.
Tatizo langu lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na imani potofu zilizokua
zimetawala kwa kipindi hicho. Baada ya kuugua surua ilisemekana kua huyu mtoto
(mimi) hatakiwi kuonekana kwa watu hivyo niliwekwa ndani. Badae mama ndo
alikuja kugundua kua macho yalikua yanaharibika baada ya kufungua kope za macho
yangu, badae wakaamua kunipeleka hospitalini lakini walikua wameisha chelewa.
Nilibahatika kusoma mpaka elimu ya sekondari
lakini sikufanikiwa kuendelea zaidi kwasababu ya gharama za masomo pamoja na
ukosekanaji wa vifaa. Kwasasa naishi na mama yangu sijaoa wala sina mchumba.
Changamoto kubwa ninayo kumbananayo ni
upatikanaji wa mahitaji muhimu ya kuniwezesha kuishi kama mwanaadamu wa
kawaida, kwamfano; chakula, malazi na mavazi inakua vigumu sana kuvipata hasa
pale unapokua huna shughuli ya kukupatia kipato.
Wakati mwingine sio rahisi sana kukubalika
katika jamii. Inachukua muda mrefu kwa jamii kuja kukukubali, labda waone tu
umefanya kitu flani ambacho kinawezakua ni kivutio kwao. Kwamfano; Niliwahi
kumwelekeza jamaa mmoja aliyekua anatafuta duka flani hapa Musoma, nikamwambia
kua twende mimi ntakupeleka lakini hakutaka kuniamini. Sasa hii ni sehemu ya
changamoto ninazo kumbananazo sababu kile ambacho mi nakitenda hakiataaminika
mpaka mwenye macho akithibitishe kwamba ni kweli nakiweza ama sikiwezi. Kwahyo
kukubalika kwangu kutategemea uwezo wangu katika kukiweza hicho kitu. Hii
inapelekea mambo mengi kua magumu kufanyika sababu sio kitu kizuri kumwambia
mtu kua hiki kitu ntakufanyia halafu asiwe na imani!.
Changamoto nyingine iko katika swala la fimbo
nyeupe ambazo ni chache. Pamoja na kua chache bado hazitoi ishara kukufahamisha
kama kuna kitu flani mbele yako ambacho unatakiwa kua tayari kukikabiri, hii
inapelekea ugumu flani katika kutembea kwa watu wasio ona. Kama kungekua na
uwezekano basi tungeweza kupatiwa fimbo zenye uwezo huo ili tuweze kutembea
salama na kwa uhakika.
Nilikua na ndoto zakuja kua mwanasheria au
mwalimu lakini sijafanikiwa kuzifikia ndoto zangu. Pamoja na kusoma kwa
changamoto nyingi sana hasa katika elimu ya msingi ambapo ilikua inakulazimu
kuwategemea watu wakusomee ili uweze kuandika lakini bado nilikua na ndoto za
kuendelea na nilifanya hivo. Nilianza kupata shida kubwa sana kipindi
nilipoingia sekondari, ilikua inamlazimu mtu awe na pesa ili amtafute mtu
umpatie fedha ili akusomee na wewe uandike. Kwasababu kinachofanyika sekondari
baada ya mwalimu kufundisha na kuandika notisi huwezi kusomewa humohumo darsani
kama ilivokua shule ya msingi. Inakubidi baada ya vipindi umtafute mtu mwenye
macho kwa muda wako na pesa yako mwenyewe ukaenae kwenye chumba maalumu
akusomee na uanze kuandika masomo ya siku nzima. Pamoja na hayo, karatasi
(kwaajili ya kuandikia watu wenye ulemavu wa macho) zinakua ni duni maana
upatikanaji wake ni tatizo, kunawakati zinaweza kukosekana mpaka kipindi cha
mwezi mzima na kwakipindi hicho chote walimu wanaendelea kufundisha na notisi
zinaongezeka pia. Kwahyo utakapoanza tena kuandika masomo tisa utakua umepoteza
muda mwingi sana kiasi kwamba hata muda wakujisomea unakua hadimu pia.Hivyo
inakupatia mzigo mkubwa tena wa kukisoma kitu ambacho kilisha fundishwa muda
mrefu uliopita na wakati huohuo kukisoma kitu kilichofundishwa kwa wakati huo. Hali
hii inasababisha walemavu hasa wasioona warudi kua ombaomba katika mitaa
mbalimbali ya nchi hii.
Naiomba jamii iweze kuwathamini na kuwasaidia
watu wenye ulemavu kwasababu watu wenye ulemavu hususani wasioona wanaishi
katika mazingira magumu sana. Asiyeona asipokua na pato lolote anapata taabu
sana. Naiomba jamii iwe tayari kuwasaidia watu wenye ulemavu, nafahamu kua kuna
wenzetu ambao sio waaminifu lakini kama hao watu wakikutokea na ukafahamu
mwachie Mungu tu kwakua wewe umeishatoa. Pia naiomba jamii ishiriki kikamilifu
katika kuwasaidia watu ambao wako katika mazingira yanayoweza kuwapelekea kua
walemavu ilikusudi waepukane na hali hii ya ulemavu kwani ni tatizo kubwa mno.
Watu wenyeulemavu wenzangu nawashauri
tuendelee kujitahidi pale tunapokua tumepata nafasi mbalimbali kama shule au
ajira ili tuweze kujiendeleza. Pia kile ambacho tunakipata kama misaada inatakiwa tukitumie kwa uaminifu mkubwa ili
mtu anapokuja tena kuangalia kile unachokifanya akute umefanya vizuri. Kwahyo
nivyema tukafanya kazi kulingana na uwezo aliotuwezesha Mungu, tusilemae tu kwa
kisingizio cha ulemavu.
Naziomba asasi mbalimbali hasa zile
zinazojishughulisha na maswala ya watu wenye ulemavu zifanye kazi zake
kulingana na lengo la kuanzishwa kwake, wasitumie vibaya misaada wanayopewa.
Pia wajitahidi kuvumbua vitu mbalimbali vinavoweza kuwasaidia watu wenye
ulemavu sio tu kuendelea kutoa habari kuhusu haki zetu.
Serikali yetu ijitahidi sana kutekeleza
wajibu wake. Tunazo rasilimali nyingi sana ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza
kuwasaidia watu wenye ulemavu. Hivyo rasilimali zilenge makundi yote. Misaada
itolewe kwa vyama vya watu wenye ulemavu ilikusudi hata watu wenye ulemavu
waweze kukopa kupitia vyama vyao wenyewe. Pia vilevile katika zile nafasi kumi
(10) za wabunge wa kuteuliwa zingetolewa nafasi kwaajili wa vyama vya watu
wenye ulemavu kuteuliwa ili tuweze kupata wawakilishi katika vyombo vya kufanya
maamuzi.
Nawaomba sana ndugu zangu wasioona ambao wako
mashuleni wajitahidi sana kusome kwabidii pamoja na changamoto nyingi
wanazokumbana nazo.
Read More ->>