Naitwa Mgosi Chacha, naishi Musoma mjini
katika mtaa wa mkendo. Nina ulemavu wa viungo, kwasasa sijafanikiwa kuwa na
familia bado natafuta maisha.
Nilizaliwa nikiwa mzima kama watu wengine, ila
baada ya kufikisha umri wa miaka miwili nilipatwa na maradhi ya kienyeji,
ambayo kimira yalikua kama miiko kwetu. Baba alikutana na vitu flani ambavyo ni
miiko kimira, kwahiyo mi nilipozaliwa ndo nikapatwa na hayo maradhi. Baba na
mama walikosa ushirikiano katika swala zima la kuniuguza mimi, hii ilimpelekea
mama kunihudumia jinsi anavojua mwenyewe hatimaye ndo nikapata ulemavu.
Changamoto kubwa ninayo kumbananayo ni
ubinafsi uliojikita katika jamii. Kwamfano mtu kama mimi nina elimu ya ufundi
(welder) na nimesoma chuo kabisa, lakini nikifika ofisini kwa mtu kuomba kazi
sipewi kazi. Nakataliwa na kutimuliwa katika mazingira yao, pamoja na
kuwaonesha vyeti vyangu kama uthibitisho wa uwezo wangu katika kuifanya kazi
hiyo. Nikutokana na hali ya ulemavu nilionao jamii hunichukulia kama mtu
asiyeweza kufanya kazi. Na hii ndo ilinipelekea kuamua kujiajiri na kufanya
kazi ya kushona viatu.
Naishauri jamii kutuangalia sana sisi watu
wenye ulemavu na wasitutenge sababu kulemaa viungo sio kulemaa kila kitu cha
mwili wako. Jamii ijitahidi kuwa karibu sana na sisi kwasababu sisi ni kama wao
na wao nikama sisi.
Nawashauri watu wenye ulemavu
kuondoa ile kasumba ya kutokutaka kujitegemea kwasababu ya ulemavu walionao. Mlemavu
anawezakuwa na familia na akategemewa kama watu wengine. Mlemavu sio mtu wa
kutegemewa kusaidiwa kwa kila kitu, inabidi kujisaidia wakati mwingine. Ukiwa
umelemaa viungo tu na unaakili ya kukuongoza katika mambo mengine kwanini
usijitegemee?
Naona kwa wakati huu serikali imeanza kutupa matumaini ya
kutukumbuka, hapo awali tulikuwa tumesahaulika kabisa. Nashauri serikali
kuziboresha ofisi zake ili ziweze kufikika na watu wa aina zote pasipo
kuwabagua watu wenye ulemavu (hususani walemavu wa viungo). Hii itatuondolea
ile adha ya kuwaagiza watu wakatuzungumzie haja zetu na badala yake tutaweza
kujieleza wenyewe.
Mashirika ya watu binafsi
kidogo wana uelewa, hata wakiamua kufanya kitu wanakifanya kwa kuzingatia maoni
ya wadau mbalimbali. Nayashauri mashirika na taasisi mbalimbali kushiriki
katika kuhakikisha walemavu mbalimbali (ambao wengi wao hawana elimu) wanapatiwa
haki zao za msingi.
Read More ->>