YOHANA
MAGAYI
Naishi katika wilaya ya Bunda mkoa wa Mara,
nina mke na watoto.
Kazi yangu ni ufundi seremala fani niliyoipata katika chuo
cha walemavu Yombo Dar es salaam mwaka 1985
- 1986 na pia Milongo Mwanza 1988 – 1989. Pamoja na hayo nilipata
mafunzo ya utetezi wa haki za binaadamu kwa watu wenye ulemavu kutoka ICD,
kwahyo mimi ni mwanaharakati pia.
Kwa mujibu wa maelezo ya wazazi wangu,
nililemaa baada yakuwa nimeanza kutembea nikiwa na umri wa miaka miwili (2).
Niliugua polio iliyonipelekea kukaa kwa muda mrefu na baadae kunisababishia
ulemavu kwa ujumla.
Nilipata changamoto kubwa katika kuliendea
swala zima la kuoa, hata yule niliyekua natarajia kumuoa kabla alishtuka
kusikia kua mimi mlemavu nataka kumuoa! Alifikiri kua tutazaa watoto wenye
ulemavu pia. Baada ya mimi kupata mtoto wa kwanza mwaka 1988, aliniandikia
barua kwamba sasa niko tayari kuolewa na wewe kwakua sikutegemea kama ungekuja
kuzaa watoto wazima. Namshukuru sana mke wangu wa sasa kwa uvumilivu tangu 1988
mpaka leo.
Swala la kuoa au kuolewa nichangamoto sana
kwa watu wenye ulemavu wapo wengi wanaotamani kupata wenzi wao lakini
inashindikana sababu ya ulemavu walionao. Wengine wanapata wenzi lakini jamii
zao zinaendelea kulalamika kwa kuona mtu asiyekua mlemavu akiolewa na mlemavu.
Kuna vikwazo vingi katika kupambana na
maisha, kwa ujumla mimi ni Mwenyekiti wa kijiji na niligombea na watu wazima
wenye viungo vyao vyote, jamii ilinielewa na kunichagua kuwaongoza. Lakini bado
napambana na vikwazo vingi kwasababu kuna watu wanajitokeza na kuuliza maswali:
‘Hivi watu wa jamii hii hawana akili kabisa, inawezekanaje watu zaidi ya 5000
mkakubali kuongozwa na mlemavu, hamuoni kwamba huu ni udhaifu mkubwa?’. Wakati
mwingine swala la kupata kipato kwa mtu mwenye ulemavu imekua ni changamoto
sana. Kwa mfano sisi tunaoishi katika mkoa wa Mara ambapo shughulikubwa ya
kipato ni kilimo, kitu ambacho kwa udhaifu wetu hatuwezi. Shughuli ya pili ni
Uvuvi ambayo pia ni ngumu kwetu, kwahyo unakuta kupata kipato ni ngumu sana.
Nashukuru kwa kazi yangu hii ya Useremala japokua ni ngumu lakini natenda na
ninapata mahitaji. Nayashukuru pia mashirika haya ya ICD na mashirika mengine
ambayo tunapokutana yanatupa changamoto za namna ya kujitegemea kuliko
kutegemea misaada.
Mwanzoni kabisa nilikua na fikra ya ufundi toka
mwanzo na ilikua ya jadi kwasababu hata baba zangu walikua wachongaji. Baadae
baada ya kuingia shule nilitamani sana kua mhasibu, lakini ndoto hiyo haikufika
baada ya kukosa mtu wakuniendeleza katika masomo pamoja na uwezo mkubwa
niliokuanao darasani. Kwakweli mzee wangu alipata udhaifu wa kifikra, aligoma
kabisa na kusema kwamba wewe hata nikikusomesha hutoweza kwenda kokote.
Namlaumu sana kaka yangu ambaye alikua Dar es salaam wakati huo. Nilimwomba
anitafutie nafasi ya kurudia mitihani lakini hakuweza kutekeleza hilo.
Nilipokwenda Yombo nilitegemea ningepata nafasi ya kusomea uhasibu lakini baada
ya kuikosa nikaamua kujiingiza kwenye ufundi kama ndoto yangu ya kwanza
ilivokua. Nashukuru kwamba leo hii inanisaidia sana
kwakweli. Imenitunza na kunipa mafanikio makubwa, mpaka sasa nina watoto saba
(7) na watatu kati yao wamefikia elimu ya sekondari na ninasomesha wengine
hakuna mtoto ambaye amenishinda. Nimefikia malengo yangu kwakweli maana
namtunza mke wangu nawatunza watoto wangu pia na sijawahi kumpa mtu kunilelea
mtoto hata mmoja kati ya hao saba wote.
Naishukuru sana jamii ya kijiji ninamo ishi,
mpaka kufikia kunipa hadhi yakuwa mwenyekiti wa kijiji ni jambo la kushukuru
sana kwakweli, inamtizamo wa pekee kabisa, kitu ambacho hata Rais hana mtizamo
huo. Naishauri jamii kwa ujumla kuwaamini na kuwaheshimu watu
wenye ulemavu, kilicholemaa ni baadhi ya viuongo tu, kitu kinachofanya kazi
kumudu maisha ya mtu hasa ni akili, kwahyo tunaweza tukiwezeshwa.
Jamii itambue kwamba sisi ni moja kati ya jamii inayofanana nao.
Naishauri serikali kupunguza ule udumavu
ilionao. Kwa mfano; kuna sheria ya watu wenye ulemavu lakini wameidumaza tu
tangu ilipo pitishwa mwaka 2010 mpaka leo haijatungiwa kanuni. Mpaka tunaelekea
katika katiba mpya bado sheria ile haifanyi kazi na bado sina imani kama
itafanyakazi. Naishauri serikali ihakikishe sheria ile inapata kanuni na
kufanya kazi. Pia walemavu wapatiwe nafasi za kujiendeleza. Nashauri pia serikali ivifungue na kuviendeleza vyuo vya watu
wenye ulemavu. Kwa mfano chuo cha Milongo Mwanza kimefungwa kasababu ya kukosa
walimu wakati serikali ina bajeti.
Nayashauri mashirika yasiyokua ya kiserikali
kama ICD, CCBRTna mengine mengi kuongeza juhudi sababu ndio yaliyosababisha
watu wenye ulemavu kutambua haki zao. Nayashauri yaendelee kupiga kelele kwakuwa
ndiyo yaliyotupatia mwanga, kwakuwa serikali imeweka kabatini sheria na
taratibu zote za kumpatia mtu mwenye ulemavu huduma na haki zake.
Read More ->>