HOTUBA YA MGENI RASMI
WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII
MHESHIMIWA DKT.HUSSEIN ALI MWINYI (MB)
KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA
MAANDISHI YA BRAILLE TAREHE 4 JANUARI, 2013
·
M/kiti wa Taasisi
ya Huduma na Maendeleo kwa Wasioona Tanzania
·
Ndugu Viongozi,
Wadau na Wanachama wa Taasisi ya Huduma na Maendeleo kwa Wasioona,
·
Wananchi wote
mliohudhuria hapa, Mabibi na Mabwana.
Kwanza
kabisa napenda kuwatakia heri ya mwaka mpya 2013. Pili napenda nichukue fursa
hii kuwashukuru kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii muhimu sana
katika kuenzi mchango wa mgunduzi wa maandishi ya Braille ambayo yameleta
ukombozi mkubwa wa maisha ya wasioona ulimwenguni kote. Wizara yangu inapenda
kuipongeza Taasisi ya Huduma na Maendeleo kwa Wasioona Tanzania (TNIB) pamoja
na wadau wote wa masuala ya watu wasioona kwa kuamua kuiadhimisha siku hii hapa
Tanzania kwa mara ya pili.
Nafahamu
kuwa Mataifa mengine Duniani yamekuwa yakiadhimisha siku hii miaka mingi
iliyopita, hata hivyo wahenga husema kuwa kawia ufike, hivyo na sisi
tumekwishaungana na Mataifa hayo na tutaendelea kuienzi siku hii muhimu.
Ndugu Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kulipongeza Kanisa la
Anglikan Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuanzisha shule kwa ajili ya Wasioona.
Aidha nayapongeza madhehebu mengine pamoja na Serikali kwa kufuata mfano huo,
jambo ambalo limesaidia sana kubadili mtizamo hasi na potofu dhidi ya watu
wasioona kuonekana kwamba hawana mchango wowote katika maendeleo ya Taifa na Jamii
zao. Wasioona ni nguvu kazi ambayo haina budi kuendelezwa kwa faida yao na
Taifa kwa ujumla. Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na kutoa msaada
kwa Asasi mbalimbali zinazojihusisha na uboreshaji wa maisha ya watu wasioona
nchini. Hii inathibitishwa na hatua ya Serikali ya kutengeneza Sera na Sheria
maalum ya watu wenye ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010. Hatua hii itasaidia sana
kuhakikisha kwamba haki za msingi za wasioona na watu wenye ulemavu kwa ujumla
zinalindwa na kutekelezwa.
Serikali
imeishatunga Kanuni za Sheria hiyo, hivyo ni kazi ya Serikali na Asasi zote za
watu wenye ulemavu kuwaelimisha wadau wao kuifahamu sheria hii na kudai haki
zao kisheria.
Ndugu Mwenyekiti, napenda niwapongeze sana Wasioona wote kwa kutumia
fursa zinazotolewa na Serikali na Asasi za Kiraia katika kujiendeleza Kielimu
na Kiuchumi. Wasioona wengi wanavyo vipaji
na uwezo katika nyanja mbalimbali ambavyo vikitumika vizuri Taifa linaweza
kunufaika kwa vipaji vyao. Kwa kutumia sheria ya Watu wenye Ulemavu, Wizara
yangu kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali itaweka mikakati endelevu
itakayowezesha watu wenye ulemavu kufurahia maisha yao kama raia wengine. Pia
napenda niwahakikishie kuwa Baraza la watu wenye ulemavu litaundwa haraka
iwezekanavyo pamoja na kuzindua mfuko maalum wa watu wenye ulemavu ambao
utasaidia sana kuwezesha shughuli zenu kuendeshwa kwa uhakika.
Ndugu Mwenyekiti, nafahamu kua mko katika mchakato wa kuanzisha mradi
wa Kiwanda kidogo cha kutengeneza fimbo nyeupe zinazotumiwa na Wasioona.
Serikali kupitia Wizara yangu iko tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha kwamba
mradi huu unafanikiwa. Fimbo nyeupe imetambuliwa rasmi kisheria katika Sheria
ya watu wenye Ulemavu, hivyo ni wajibu wa Wizara yangu kuona kwamba mpango huu
unafanikiwa. Kwa kuunga mkono jitihada zenu napenda kutoa changamoto kwa watu
binafsi, mashirika na Serikali kwa ujumla kuona umuhimu wa kuchangia mradi huu.
Ndugu Mwenyekiti, kuhusu changamoto zinazowakabili katika upatikanaji
wa vifaa na machapisho mbalimbali katika Breille, Wizara yangu itashirikiana na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia
Tamisemi kuzipunguza changamoto hizi. Ninawaomba wasioona wote hususani wenye
umri wa kwenda shule wapelekwe shuleni na wale ambao umri wa kwenda shule
umepita wapelekwe katika vyuo mbalimbali vya mafunzo ili kuwapatia stadi na
ujuzi wa kuwawezesha kujitegemea. Pia napenda kutoa wito kwa wananchi wote
kuhakikisha kwamba wanatunza Afya ya macho yao na wanapoona kuwa wanasumbuliwa
na matatizo ya macho wasisite kwenda katika Hospitali zilizo karibu nao.
Kwakufanya hivyo wataweza kubaini haraka na kuepusha athari zinazoweza
kuwasababishia kutoona.
Ndugu Mwenyekiti, mwisho napenda niwapongeze sana kwa kuandaa
maadhimisho haya na pia niwashukuru wadau mbalimbali waliochangia kwa hali na
mali kufanikisha maadhimisho haya. Naahidi kuwa kuanzia maadhimisho yajayo
Wizara yangu itaendelea kuchangia katika kufanikisha maadhimisho haya.
Napenda niwashukuru tena kwa kunialika kuwa Mgeni
rasmi katika maadhimisho ya mwaka huu. Nawatakieni mafanikio mema katika
shughuli zenu na heri ya mwaka mpya 2013.
Asanteni
sana kwa kuniskiliza.
Read More ->>