Monday, March 11, 2013

‘Njia bora ya kupambana na changamoto zinazotukumba watu wenye ulemavu ni kuonesha uwezo wetu kwa vitendo.’ ABDILLAH OMAR ABUBAKAR

0 comments


Naitwa Abdillah Omar Abubakar, ni mweka hazina wa chama cha Albino Tanzania (TAS) na pia ni mjumbe wa bodi ya SHIVYAWATA.

Namshukuru Mungu nimeoa na nina watoto watatu (3). Mke wangu ni Albino vilevile ila sio kwamba nilimuoa kwasababu nisingeweza kupata mwanamke wa aina nyingine. Ni mapenzi tu ndo yalitufanya tuoane. Vikwazo katika jamii huwa havikosi, hususani vikwazo vya kimtizamo. Kila mzazi anatamani mwane apate kilicho bora, huo ndo ukweli.
Nilipowambia wazazi wangu kua naoa na nikawatajia mchumba wangu, hawakuweka shaka kua kwanini namuoa yeye? Halikadhalika wazazi wa mwenzangu hawakuweza kuniwekea vikwazo pia. Inawezekana watu wa nje ambao sio wazazi wetu kuanza kujiuliza maswali. Hili ni swala la kawaida tu. Lakini baada ya kuoana tunaishi na jamii katika mazingira ambayo ni mazuri mno! Hatukumbani na unyanyapaa wa aina yoyote. Tunashiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na tunathaminiwa katika kila ngazi.
Changamoto zilizojaa katika jamii ni zile za mitazamo. Unaweza ukafika mahala, watu kwa kukuona kwamba wewe ni Albino wanadhani hata ule uwezo wa kufikiri huna. Mara nyingi kupambana na changamoto hizi ni kutumia njia ya kuonesha kwa vitendo. Kwamba pale ambapo unaona kuwa kuna kikwazo cha aina flani, basi wewe unaonesha uwezo ili kukinzana na kile kikwazo. Kwahiyo majibu yanapotokea, ushirikishwaji na kuaminika hupewa nafasi kubwa sana. Lakini naweza nikasema kwa uzoefu wangu wa maswala ya watu wenye ulemavu, nimepata kuskia na kuona mambo mengi ambapo, kama kusingekuepo na hivi vyama mimi nisingejifunza vitu vingi. Na kwabahati nzuri ndani ya familia yangu sikuwa na unyanyapaa tokea nilipozaliwa mpaka nakua. Kwahiyo mambo mengi nisingeweza kuyafahamu. Wazazi wangu waliamini kuwa mimi nahitaji kua chini yao kwa maisha yangu yote. Ispokua kutokana na kutokua na elimu nzuri ya maswala haya, kuna mazingira mengine ya malezi walionipa mimi ambayo yalikua ni vikwanzo kwangu ila hawakujua.
Moja ya ndoto zangu kubwa ilikua ni kutoka kwenye jamii na kufahamika, kutambulika na kusikika pia ili kutoa mchango ndani ya jamii inayo nizunguka. Hizo ndoto zimejitokeza ambapo kwa sasa ni kiongozi tena kiongozi wa kitaifa wa chama na vilevile kiongozi wa shirikisho ambalo linashikilia vyama vyote vya maswala ya watu wenye ulemavu. Hivyo ndoto zangu zimeweza kutimia kwa kiasi flani.
Moja ya ndoto zangu ilikua ni kutokujiangalia nilivo ila nione je nina uwezo gani katika kutenda? Kwa mfano mimi ni Albino, kwahiyo ninapozungumza sizungumzi kama albino, ila nazungumza kama binaadamu mwenye utashi na fikra.
Maoni yangu yatajikita sana katika kauli mbiu ya mwaka huu ‘Ondoa vikwazo ili kujenga jamii jumuishi’. Vikwazo vilivyoainishwa hapa ni vingi, vikiwemo vile vya kisaikolojia. Kwamba unapomwona mtu mwenye ulemavu, ukaanza kumwona kwamba si kitu utambue kua hata yeye atajiskia kua si kitu.Hali hii inawafanya watu wenye ulemavu kujiona kwamba wao si sahihi pale walipo. Hiki ni kikwazo cha kwanza kinachojenga vikwazo vingi huko mbele ya safari. Vikwazo hivi humfanya mtu mwenye ulemavu hata awapo darasani asiweze kujiona kama mtu anayeweza kusoma hivyo kushindwa kumudu vitu vingi. Katika sehemu za mjumuiko mtu mwenye ulemavu akienda kucheza dansi watu wakashangaa, atajiona kama kichekesho na sio mtu wa kawaida. Ile hali ikiendelea inapelekea kudumaza akili za watu wenye ulemavu. Kwahiyo naiomba jamii kuondoa vikwazo hivyo.
Vikwazo vingine viko katika upande wa afya; kwa mfano kundi la albino. Hawa ulemavu wao uko katika ngozi na macho, ngozi zao hazina uwezo wa kuhimili mionzi ya jua kutokana na ukosefu wa melanini. Sasa hawa watu wanaathirika na jua kali, lakini elimu ya afya kwa wazazi wanao wazaa albino kwenye mahospitali bado iko duni. Hakuna wakunga wa kutoa elimu juu ya namna ya kuwatunza watoto wa aina hiyo. Mtoto anapofikia ule uwezo wa kuona utakuta mzazi pasipokujua anamtuma achukue kitu flani ambacho yeye hakioni. Sasa asipo kileta wanamchukulia kama mjeuri, hivyo hujikuta wanamfanyia harasi sana kitu mabacho hakimpelekei mtoto kujifunza. Watu wa afya wangetoa elimu kwa jamii juu ya albino na namna ya kuishi nao katika jamii ilikusudi nao waweze kuishi kwa amani kama watu wengine.
Ukienda mbele katika huduma za mashuleni, albino wanahitaji nyezo maalumu za kukuza maandishi ili waweze kuona na kusoma kama watoto wengine. Hiki ni kikwazo kwasababu vitu hivi hakuna. Kwamfano hata kwenye maswala ya habari za kuchapishwa kama magazeti, utakuta mtu anaishia kusoma kichwa cha habari pekeake lakini hawezi kuendelea kusoma maandishi mengine maana hana nyenzo za kuyakuza. Hivyo ni muhimu sana kuwa na nyenzo za kutosha ili albino waweze kujifunza na kupata habari mbalimbali.
Mwisho; nawaomba waajiri waondoe unyanyapaa na fikra potofu linapokuja swala la ajira kwa watu wenye ulemavu. Hii itawapelekea watu wenye ulemavu kukuza vipato vyao na kujimudu wao na familia zao hivyo kujenga heshima zao ndani ya jamii.
Read More ->>
 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |