Naitwa
Kigombe Magige ni mwenyekiti wa watu wenye ulemavu wilaya ya Bunda, naishi
katika kijiji cha Manyamanyama Bunda. Nina mke na watoto wanne (4), elimu yangu
ni elimu ya sekondari niliyo hitimu mwaka 1993 katika shule ya sekondari Ikizu.
Kwahivi sasa nashughilika na shughuli za kushona viatu pamoja na shughuli
nyingine ndogondogo za kujikimu kimaisha.
Mimi
ni mlemavu wa viungo, ulemavu huu niliupata nikiwa na miaka mitatu (3) nadhani
ilikua ni polio kwasababu mzazi wangu alinambia kua niliugua homa kali ghafla,
badae wakaenda kunichoma sindano baada ya kurudi mguu wa kulia ukawa unakataa
kufanya kazi. Walijaribu kuwa wanachimba shimo na kunisimamisha ndani kwa siku
nzima lakini hamna nafuu, matokeo yake miguu yote ikapooza na nikaishia kuwa
hivi.
Nilikutana na changamoto mbalimbali katika swala la kuoa, mke
wakwanza niliyemwoa nilikaanae baada ya siku watu wakaanza kumcheke na
kumwambia wewe utaakaje na mtu mwenye ulemavu? Baada ya muda baba mkwe na mama
mkwe wakaamua kunisaliti na kumwondoa kwangu na akachukuliwa na bwana mwingine
ambaye mpaka sasa wanajificha.
Baadae nilipata mke mwingine na kumwoa, kidogo yupo lakini
changamoto haziishi, anasema wanamcheka na kumwambia wewe nikama ‘Msimbe’
sababu mme wako mwenyewe ni kilema sijui ulimpendea nini? Changamoto
kama hizo hazikosi maana katika jamii sio wote wanaoelewa kuwa ulemavu ni
mapenzi yake Mungu, leo unaweza kuwa mzima baadae ukawa mlemavu. Wengine
wanaona ulemavu kama ni balaa katika jamii, kwakweli tuna kumbana na changamoto
kubwa katika jamii pamoja na serikali, tunanyanyaswa kwakweli.
Manyanyaso
yanakuja kwasababu ukienda serikalini hata kuomba namna ya kuwezeshwa ili uweze
kuboresha kazi zako serikali wanakwambia hawana fedha. Ukienda katika benki
wanakwambia una nini cha kuweza kujidhamini ili tukupe fedha? Ukienda kwenye
asasi hizi zinazotoa mikopo wanasema mlemavu!? Huyu anataka achukue fedha ale
apotelee kwasababu hana aseti inayoweza kumdhamini aweze kukopa. Sasa mara
nyingi watu wenye ulemavu tumekua ombaomba kutokana na kukosa mitaji yakuweza
kujiajiri sisi wenyewe, pia serikali haitupi ajira wala kupanga mafungu
kwaajili ya watu wenye ulemavu, tumekua ni watu tuliosahaulika, tunaongelewa
katika magazeti na redio lakini kivitendo hatumo kabisa.
Ndoto
zangu nyingi sijazifikia, nilikuwa na makusudi kwamba ntakapo kuwa mtumzima
niwe na familia, nipate maisha ya kujitegemea niwe na nyumba niwe na biashara
zangu nzuri zakufanya. Watoto nimeishapata na mke ninae, tatizo linakuja kwenye
ajira na biashara zangu (hasahasa kujiajiri mi mwenyewe). Sijapata mtaji
wakutosha wakunifanya nijiajiri mwenyewe, sijaweza kuajiriwa na mtu, kwa hali
hiyo bado naishi kwenye nyumba duni ya kupanga. Ukilinganisha gharama za maisha
ya kupanga, unakuta chumba wanataka elfu ishirini (20000), sasa sisi watu wenye ulemavu
tunapoenda kutafuta nyumba za kupanga kwa mtu, unakuta huyo mtu anaanza kuwa na
wasiwasi kama mlemavu anaweza kulipa kodi, mwingine atataka akupe banda tu
uishi kwasababu anaweza kukuvumilia uishi bure kwenye banda kwasababu hawezi
kukuweka kwenye nyumba nzuri ambayo anawezakuitumia kupata fedha. Hali hii
imekua ni ngumu kwangu mpaka sasa inanipa mawazo sana.
Nawashauri
wenzangu watu wenye ulemavu wasife moyo, wawe na juhudi za kutafuta fedha na
maisha wajitolee kujitumikisha ili waondokane na unyanyapaa huu tunaoupata. Pia
watu wenye ulemavu tusijishushe sana kuwa hatuwezi kitu, tuwe na nia na imani
kua tunaweza iwapo tukiwezeshwa, tusifike mahala kutegemea kwamba tuwe
ombaomba. Wale ambao tunaujuzi tujitahidi kuutumia ujuzi wetu katika kujisaidia,
tusiendelee kuwa mitaani na vibakuli tukiombaomba matokeo yake tunatukanwa
tunanyanyaswa na kukerwa na jamii. Nawale wanaoenda shule wajitahidi kusoma kwa
bidii kwasababu swala la ulemavu sio kitu cha ajabu ni maumbile tu yanayotokana
na mapenzi ya Mungu.
Jamii
ione tatizo la ulemavu ni la watu wote na jamii kwa ujumla,ione mlemavu kama
mtu anayestaili upendo na kusaidiwa ili aweze kujimudu kimaisha. Jamii ione
ninamna gani inaweza kumsaidia mtu mwenye ulemavu kua na maisha bora ili ajione
kama watu wengine. Jamii ichukulie ulemavu kama si laana au dhambi, iuone
ulemavu kama mapenzi ya Mungu. Isiwanyanyase wala kuwatenga, kwamfano unakuta
kwenye familia nyingine walemavu wanafungiwa ndani na kufichwa hawataki
waonekane, wanaonakwamba wewe ni kitu cha ajabu. Inawezekana mtu akawa
anatembea mzima lakini akawa mlemavu kuliko huyo mklemavu anayetengwa.
Asasi na taasisi zinazojishughulisha na
maswala ya watu wenye ulemavu zifanye utafiti na kuwasaidia kikweli watu wenye
ulemavu, isiwe kuwatumia watuwenye ulemavu kama chambo cha kupatia fedha na
kutumia wenyewe hiki sio kitu kizuri. Kama ni asasi imeamua kuwasaidia watu
wenye ulemavu iwasaidie kwa juhudi zote, iwapatie nyenzo za kutembelea, iwape
mikopo ya kuwawezesha kujishughulisha na uzalishaji mali, isichukulie kwamba
mlemavu ni mtu wa kulishwa tu. Asasi nyingi zinawachukua watu wenye ulemavu na
kuwakusanya pamoja kwa kuwapatia mahitaji ambayo sio ya kimaendeleo na hapo
wanakua wamewanyanyasa watu wenye ulemavu badala ya kuwasaidia kwasababu
hawawaoneshi picha halisi ya maisha yakuweza kujitegemea.
Serikali imekua na danganya toto,
maranyingi imekua ikisema kuwa inategema mafungu kwaajili ya watu wenye ulemavu
lakini haifanyi hivyo kihalisia. Ukija kwenye sheria ya mwaka 2010 ya watu
wenye ulemavu, hiyo sheria imetungwa lakini hakuna mlemavu anayejua hiyo sheria
inasema nini? Imebaki tu kwenye makaburasha yao. Serikali hiyohiyo inasema
inawawakilishi wa watu wenye ulemavu bungeni, lakini wawakilishi hao wanatoka
maofisini na kwenye vyama vya siasa na kwenda kwenye bunge! Hawajatoka kwenye
bunge na kuja kukaa na watu wenye ulemavu na kujua walemavu wanataka nini,
wanashida gani? Na kero hizo zikapelekwa bungeni, imekua watu hawa wanatetea
maslahi ya vyama vya siasa na watu walio wateua. Kwahyo tunafikiri kwamba serikali
haijatenda haki kwa watu wenye ulemavu kuwapa uwakilishi. Serikali ilisaini mkataba wa haki za
binaadamu kwa watu wenye ulemavu, lakini imekua kama danganya toto, katika
mkataba huo unaonesha wazi kwamba hata baiskeli inatakiwa inastahili serikali isaidie
watu wenye ulemavu lakini cha ajabu serikali haifanyi hivo badala yake
wanaziachia asasi. Sisi sio wa asasi sisi ni watanzania na serikali inawajibika
kwa watu wote, hakuna mafungu.
Rais naye anaonekana kuwanyanyapaa watu
wenye ulemavu kwasababu; hakuna mlemavu anayeteuliwa kua mkuu wa wilaya,
waziri, wala mkuu wa mkoa wote unakuta ni watu wenginewengine tu! Hivi mlemavu
hawezi kweli? Hivi hakuna walemavu wenye elimu? Wapo niwengi ila kilichopo
nikwamba tumetengwa kwavile wanasema walemavu wengi hawakusoma. Tunaendelea
kunyanyaswa na kupuuzwa hata kiongozi wa serikali anazidi kuonesha unyanyapaa
huo.
Napenda
pia kuzungumzia swala la wenzetu walemavu wa ngozi, hawa niwatu wakawaida kama
watu wengine lakini jamii imewachukulia kama ni ‘deal’, biashara na kuwafanya
waishi bila amani, wasiwasi, na hofu kubwa kutokana na rangi waliyopewa na
Mwenyezi Mungu. Swala la serikali kusema iwakusanye na kuwaweka pamoja, pia ni
sawa na kuwanyanyapaa. Tunaomba serikali itoe elimu kwa jamii kuwa watu wenye
ulemavu nisawa na watu wengine. Nakama mtu akibainika kuwa ameua mtu mwenye
ulemavu wa ngozi, naomba serikali ingeweka amri au sheria kali ya kuwanyonga
watu wa aina hiyo.
Read More ->>