Ilikuwa asubuhi moja ya mwezi wa nane
mwaka jana 2012 pale mimi na mwenzangu dada Mossi Magere tulipofika katika
kijiji cha Ugute, kata ya Isalavanu, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kufanya utafiti.
Kazi hii tulitumwa na Kituo cha Habari kuhusu Ulemavu (Information Centre on
Disability-ICD) cha jijini Dar es salaam.Lengo lilikuwa kuchunguza masuala
mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa haki za watu wenye ulemavu nchini mwetu.
Mwenyeji
wetu alikuwa na wazo jingine kabla hajatukutanisha na familia zenye watu wenye
ulemavu. Akatuomba tuongozane naye kwenda kumjulia hali binti mmoja. Nje ya
nyumba ile ya udongo mlango ulikuwa umefungwa kwa nje na kufuli, mwenyeji wetu
akachepuka kidogo pembeni na kuinua kitu fulani na kutoa ufunguo.Akafungua
mlango na kutuambia tuingie ndani. Mpaka wakati huo japo nilikuwa najua tuko
pale kufanya nini, lakini namna mambo yalivyokuwa yanaenda ikanipa mshangao
kidogo.
Tukaingia
ndani. Katikati ya chumba kikubwa kulikuwa na kitu kama kilichofunikwa na
matandiko. Stamili! Stamili! Mwenyeji wetu akawa anaita huku akitikisa na
kujaribu kufunua matandiko yale. Ndipo nikajua kuwa aliyelala pale ni binti
tuliyekuja kumwona. Hali iliyokuwa mle hakika iliniliza mimi na mwenzangu dada
Mossi Magere.
Pale
chini kwenye sakafu ya udongo alikuwa amelala binti Stamili, mwenye ulemavu wa
viungo. Kila mwenyeji wetu alipojaribu kumwongelesha alikataa na kujaribu
kujifunika zaidi na matandiko yake. Hakika matandiko yale yalikuwa katika hali
mbaya kutokana na kujaa mkojo na uchafu mwingine. Kwa habari tulizozipata pale
binti yule anafungiwa ndani na mama yake mzazi kila siku atokapo kwenda
shambani au katika shughuli zingine za nje.
Binti
Stamili alikuwa katika hali dhoofu akikabiliana na upweke mkubwa wa kufungiwa
ndani masaa 24 huku akiachwa kujisaidia pale pale. Matandiko yalikuwa yamejaa
mkojo na uchafu mzito, dhahiri ikionesha hakuna huduma yoyote anayopata ili
kumweka katika hali nzuri. Nyumba ile ilikuwa ikivuja na kupitisha ubaridi mkali
wote ukimwelekea binti yule mwenye ulemavu.Cha kushangaza mama yake mzazi
halali katika nyumba ile bali anayo yake pembeni ambayo ina hali nzuri
ukilinganisha na ya Stamili. Tukabaki tunajiuliza maswali mengi ambayo yalikosa
majibu maana mama yake hatukubatika kumpata kwani alikuwa shambani.
Baadae
alikuja dada yake ambaye naye anaishi katika nyumba nyingine na tukamuuliza
maswali kadhaa. Dada yule ilibidi kumbana sana mpaka kuweza kueleza machache. Kwamba
hapo awali Stamili alikuwa anaruhusiwa kutoka nje na kutembea huku na kule
katika mazingira jirani na nyumbani ni hali ambayo ilitulazimu kuuliza maswali
mengi yaliyokosa majibu ya uhakika. Dada yake akasema pia kwamba mama yake
mzazi huenda anamfungia ndani kwa hofu kwamba asije kubakwa. Lakini hiyo sababu
haikuweza kuturidhisha. Mbona sasa binti huyu amejaa uchafu utadhani si
binadamu aliyeko pale! Tukazidi kujiuliza.
Kwa
ufupi ni kwamba Stamili ametelekezwa na familia yake, ndugu, jamaa, marafiki na
serikali hasa mamlaka ya serikali za mitaa, ikiwa ni pamoja na uongozi wa
kijiji na kata. Kwa upande wa Halmashauri ya Mufindi viongozi pale walisema
kwamba hawana taarifa kuhusu masahibu ya binti yule. Tulichofanya sisi kama
watafiti tulihakikisha tumeacha taarifa kwa afisa ustawi wa jamii pamoja na
ofisi ya elimu (msingi). Vilevile mratibu wa masuala ya walemavu katika kata ya
Isalavanu bwana Emilio Mbata tulimsihi sana afikishe kilio chetu kwa wadau wote
ili waweze kumsaidia binti Stamili.
Hivi
majuzi tarehe 17.1.2013 nikiwa Mufindi kwa mara nyingine tukitengeneza
documentary film (filamu makala?) niliweza kufika katika kijiji cha Ugute
tena.Kwa mshangao wangu hali ya binti yule bado ni mbaya na mwili wake
unatisha.Sasa hivi wadudu mwilini na harufu kali chumbani mle ni hali ambayo
hutapenda kukutana nayo. Bila shaka Stamili kama wasichana wengine atakuwa
anapata siku zake za mwezi, lakini ni msichana ambaye hayajui maji, ni hali
ngumu kuifikiria. Mama yake hatukuweza tena kumpata angalau tusikie machache
toka kwake.
Kwa
ufupi ni kwamba baada ya kurudi Mafinga (Makao makuu ya wilaya ya Mufindi
kutoka kijijini Ugute ili kuendelea na shughuli nyingine, tulikutana na Afisa
Ustawi wa Jamii (sio yule wa mwanzo) na kumweleza habari hii. Alichoahidi ni
kwamba atachukua hatua. Kwa makala hii naomba kumsihi Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri ya Mufindi ndugu Shimwela Limbakisye achukue hatua madhubuti
kuingilia kati ili binti yule aweze kupata matibabu sahihi (rehabilitation) na
kurudishiwa utu wake. Naandika hivi nikiamini kaka Shimwela atafanya hivi maana
baadhi ya watu wenye ulemavu pale
Mafinga wamemtaja kama mtu anayejali sana. Ushahidi wa video wa hali ya binti
huyu upo kama ikihitajika utolewe kuthibitisha haya kwa hatua zaidi za
kumsaidia.
Hali
kama hii ya binti Stamili ni hali halisi ya watu wengi wenye ulemavu nchini
Tanzania. Iko hivyo wakati Tanzania ikiwa tayari ilisharidhia Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu wa mwaka 2006 (The United Nations
Convention on Persons with Disabilities of 2006) na ikapitisha sheria ya watu
wenye ulemavu ya mwaka 2010 (Persons with Disabilities Act of 2010) ya Tanzania
Bara.
Masahibu
yanayomkuta binti Stamili mwenye ulemavu wa viungo ni miongoni mwa changamoto
nyingi sana dhidi ya watu wenye ulemavu mbalimbali duniani ambazo zilisababisha
Umoja wa Mataifa kuandika Mkataba wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu wa mwaka
2006.Mkataba huu ni chombo cha kisheria cha kimataifa ambacho kinazibana nchi
zilizoridhia kuhakikisha kwamba haki za watu wenye ulemavu zinalindwa. Mkataba
huu ni hatua kubwa ya kubadili mitazamo hasi katika jamii zetu kuhusu ulemavu
na kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata nafasi ya kufurahia siku za
maisha yao sawa na watu wengine.
Mkataba
huu unalenga kuendeleza, kulinda na kuhakikisha watu wenye ulemavu wanafurahia
haki zao za kibinadamu. Haki hizo ni kama vile kupata elimu, huduma za afya,
ajira, kupata habari na uhuru wa kufanya mawasiliano , urahisi wa kwenda mahali
kokote kama vile katika majengo na kupanda vyombo vya usafiri kwa urahisi,
kushiriki katika siasa, kuheshimiwa nakadhalika.
Nchi
yetu iliridhia mkataba huu mwaka 2009 na kulazimika kuanza kuchukua hatua za
kuutekeleza ambapo mwaka 2010 ilipitishwa sheria ya watu wenye ulemavu. Sheria
hii inaielekeza serikali na vyombo mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu
wanafurahia maisha kwa kupata huduma za afya, elimu, ajira, na kushiriki katika
kila jambo ndani ya jamii yetu bila kunyanyapaliwa au kusahauliwa kwa namna
yoyote ile.
Tukitazama
mfano wa binti Stamili, huyu ana wakati mgumu sana kwa sababu anakabiliana na
unyanyapaa kuanzia ndani ya familia yake.Watu wanaomzunguka kuanzia mama yake
mzazi, na ndugu wengine hawana muda naye na anakosa haki zake nyingi tu.
Anafungiwa ndani masaa 24, na anaachwa alale kwenye sakafu yenye baridi kali.
Afya yake inazifi kudhoofika siku hadi siku na bila shaka hata athari nyingine
za kisaikolojia zinazidi kumsonga. Si kiongozi wa serikali ya kijiji, kata,
wala halmashauri ya Mufindi aliye tayari kuchukua hatua kutekeleza matakwa ya
sheria ya watu wenye ulemavu ambayo ilitungwa kuwalinda watu kama Stamili licha
ya kuwa taarifa kumhusu zimetolewa mara kadhaa kwa mamlaka hizo.
Halmashauri/manispaa
za wilaya zinatajwa na sheria hii kama wadau wakubwa wa kulinda haki za watu
wenye ulemavu. Lakini jambo moja ambalo lililojitokeza katika utafiti wa ICD ni
kwamba sheria hii ya kulinda haki za watu wenye ulemavu haifahamiki kabisa na
maofisa wengi wa halmashauri na manispaa. Hata utafiti uliofanywa hivi karibuni
na Foundation for Civil Society umeonesha udhaifu huo mkubwa katika kutetea
haki za watu wenye ulemavu. Hata maofisa wa ustawi wa jamii nchini ambao pia
wanatajwa na sheria hii kama chombo kikubwa cha kulinda haki za watu wenye
ulemavu bado wengi hawaijui huku utendaji wao wa kazi ukikabiliwa na mapungufu
mengi hasa ya kibajeti.
Ili
binti Stamili na watu wengine wenye ulemavu nchini mwetu waweze kuishi kwa
furaha kama watu wengine ni lazima Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye
Ulemavu na Sheria ya Watu wenye Ulemavu vitekelezwe angalau kwa viwango fulani
vinavyotia moyo. Sheria inataka kuwepo mfuko wa kitaifa wa watu wenye ulemavu,
basi uundwe. Sheria inataka kuwepo na daftari la watu wenye ulemavu wote
nchini, lianzishwe orodha yao ijulikane na pale walipo ili iwe rahisi
kushughulikia mambo yao.
Halmashauri
za wilaya na manispaa zote nchini zitenge fedha maalumu za kushughulikia huduma
kwa watu wenye ulemavu.Mipango yao ya maendeleo ijumuishe pia masuala
yanayohusu watu wenye ulemavu (mainstreaming). Namna hiyo itakuwa rahisi hata
pale taarifa za watu kama Stamili zikifika halmashauri zikafanyiwa kazi
kirahisi kwa kuwa maofisa watajua kuwa fedha zipo.
Sina
hakika Tanzania imefikia wapi na utekeleza wa mambo yaliyoainishwa katika
Mkataba wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu. Labda kama tukiweza kusoma taarifa
ya utekelezaji inayotakiwa kutumwa Umoja wa Mataifa tutajua. Lakini vyovyote
vile ilivyo hali bado ni mbaya sana kwa watu wenye ulemavu. Unyanyapaa bado upo
mwingi tu. Shule wanakosoma watoto wenye ulemavu, ziwe zile jumuishi au zile
maalumu, bado zinakabiliwa na mapungufu mengi ya vifaa vya kusaidia utoaji na
upataji elimu. Mawazo hasi kwamba ulemavu ni janga au nuksi katika familia bado
yapo katika jumuiya zetu na yanasababisha watu wenye ulemavu kunyanyapaliwa
katika kila kona ya maisha yao. Waajiri nao wanatakiwa kisheria kutoa ajira kwa
watu wenye ulemavu angalau kwa kiwango fulani (kimetajwa katika sheria), lakini
bado kusitasita ni kwingi mno.
Njiani
kutoka kijijini Ugute, kata ya Isalavanu, wilaya ya Mufindi, kurudi Dar es
salaam, naambiwa binti Stamili bado yupo ila sina hakika lini ataweza kuonja
matunda ya uhuru unaotajwa katika sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010.
Natumaini Mufindi imenisoma.
Moses Gasana
Mawazo Chanya Media
0713480670
mosesgasana@yahoo.com
Read More ->>