Sunday, January 20, 2013

MKASA WA MLEMAVU ANAYETESEKA BADA YA KUBAKWA





Asha Musa (katikati) akiwa na bibiu yakew na mtoto wake.

SIKU hizi kuna watu wanasema; “Ni heri ukutane na mnyama mkali kama, simba au chui unaweza kusalimika, kuliko kukutana na binadamu, kwani anaweza kukudhuru.”
Maneno haya yanatokana na unyama wanaofanyiana  wenyewe kwa wenyewe.

Kila siku tunasikia unyama unaofanywa na binadamu, leo utasikia baba wa miaka 45 amemnajisi mtoto wa miezi minne, mke amemkata na shoka hawara wa mume wake, majambazi wameua familia nzima na mambo kama hayo.
Hayo yanadhihirishwa na mkasa  wa Aisha (siyo jina lake halisi), aliye na  ulemavu,  ambaye hajiwezi kwa lolote bila msaada wa mtu.

Hata hivyo, pamoja na hali aliyonayo, bila chembe ya huruma, Aisha amekuwa mwathirika wa unyama wa binadamu, baada ya kubakwa.
Binti huyo anaishi katika Kijiji cha Ntisi, Kata ya Bicha, umbali wa kilometa tano kutoka Kondoa Mjini, eneo ambalo hakuna usafiri mwingine unaoweza kukufikisha zaidi ya bodaboda.
Katika kijiji hicho hakuna asiyemfahamu binti huyo kutokana na hali yake na historia ya maisha yake, ambayo inasikitisha kila aliye karibu naye.

Kwa takriban miaka 21, binti huyo ameishi na bibi yake aitwaye Mwajabu Haji, lakini sasa familia hiyo imeongezeka, baada ya Aisha kujifungua mtoto, ambaye ni zao la kubakwa. Mtoto huyo sasa ana umri wa miaka sita.
Ukifika nyumbani kwao utamkuta Aisha amekaa katika kiti chake maalumu cha mbao, alichotengenezewa na bibi yake.
Hana kiungo chochote mwilini mwake kinachoweza kufanya kazi zaidi ya mdomo wake.

Hata hivyo, inzi humwingia mdomoni na kutoka, wakirukaruka katika mwili wake wapendavyo, kwani binti huyo hawezi kuwafukuza kwa kuwa mikono yake haifanyi kazi.
Umbile lake lilivyo
Zaidi ya kuzungumza, Aisha hawezi kufanya shughuli yoyote kutokana na kuwa, mikono na miguu vimejipindapinda.

Tumbo lake limesogea upande wa kushoto na kichwa  kulia.
Mara nyingi anapoongea mikono hupata nguvu ya ajabu ambapo huanza kurukaruka huku na kule kwa kuwa hawezi kuizuia, hujigonga na kujiumiza katika sehemu mbalimbali.

Mikono hiyo haina nguvu ya kuweza kubeba kitu chochote  au kufukuza wadudu wanaotambaa katika mwili wake hasa inzi kutokana na vidonda vilivyojaa.
Historia ya maisha yake
Aisha  alizaliwa mwaka 1990 Musoma, mkoani Mara akiwa na ulemavu. Alipofikisha umri wa mwaka mmoja, alipelekwa kwa bibi yake mzaa mama, baada ya baba yake kukataa kuendelea kumlea. “Kwa kweli ninamshukuru Mungu na bibi yangu kwa kiasi kikubwa,  kwa kuwa katika historia yangu, nimekutana na changamoto nyingi, lakini hakunitupa au kuninyanyapaa,” anasema na kuongeza:
“Ninamhurumia bibi kwa kuwa pamoja uzee, lakini hana budi kubeba, jukumu la kututafutia riziki ya kila siku kwa ajili yangu na mtoto wangu.

Natamani ningekuwa na uwezo hata wa kumsaidia kuosha vyombo,” anasema Aisha.

Anasimulia kuwa, kwa mujibu wa bibi yake, mama yake alilazimika kumrudisha kijijini hapo, baada ya baba yake kutaka wamchinje au wamtupe.
Aisha anaeleza kwamba, kwa kuwa mama yake alikuwa akiipenda ndoa yake, hakuwa tayari kumtupa au kumuua badala yake alimpeleka kwa bibi yake, ili kuokoa uhai wake.
“Mama yangu mzazi aliwahi kupigwa na baba,  huku akitishiwa kuachwa endapo atanilea, ndugu zake baba walimshauri anitupe,” anasema Aisha.

Anaongeza kuwa, hajawahi kukutana na baba yake mzazi, lakini anadai kuwa anamfahamu kwa jina la David Chacha akieleza kuwa anafanya kazi ya upishi jeshini huko Monduli.

Mama yake mzazi ambaye pamoja na kumrudisha kwa bibi yake, alikuwa akifika kijijini hapo mara kwa mara kumjulia hali, hata hivyo alifariki mwaka 2011.
Alivyobakwa mpaka kupata ujauzito
Kutokana na umbile lake lilivyo na pilikapilika za bibi wa Aisha katika kutafuta riziki, ilimchukua miezi saba bibi huyo kugundua kuwa mjukuu wake ana ujauzito.

Bibi huyo anasema kuwa aligundua kuwa mjukuu wake ana ujauzito, wakati tayari imeshafikisha miezi saba.

Anaeleza kuwa alibaini kuwa matiti ya Aisha yakiwa yamejaa, ndipo alipomchunguza vizuri na kugundua kuwa ni mjamzito.
Mwajabu (Bibi wa Aisha) anasimulia kuwa alipomuuliza Aisha kutaka kujua aliyempa ujauzito na jinsi alivyoupata, alishangaa kwa kuwa, aliyempa ujauzito huo ni binadamu mwenye akili timamu.
Anasema kuwa baada ya hapo alimpeleka mjukuu wake kliniki, lakini pia alimtafuta kijana aliyempa ujauzito, ambaye anafahamika kwa jina moja la Mashoto.
“Bibi mimi huingiliwa na mwanamume  aitwaye Mashoto, ila kaniambia nisimtaje, ikitokea nimemtaja basi atanichinja ndiyo maana nilinyamaza, nikiogopa kuchinjwa,” anaeleza Mwajabu akimnukuu Aisha alipotaka kujua aliyempa ujauzito.

Baadaye, bibi huyo aliamua kwenda polisi kutoa taarifa, ambapo aliambiwa atoe Sh500, ili mgambo watumwe kwenda kumkamata Mashoto.
Mgambo hao walifanikiwa kumtia ndani mtuhumiwa,  lakini baada ya siku chache alitoka na kuwaomba waifute kesi kwa madai kuwa atamtunza binti huyo na mtoto atakayezaliwa.

“Sijawahi kupata msaada wowote kutoka kwa mwanamume huyo tangu wakati huo, mpaka sasa mjukuu wangu ametimiza miaka sita, lakini nimeamua kumuachia Mungu,” anasema Mwajabu.
Akisimulia kuhusu ujauzito wake, Aisha anasema kuwa alipitia wakati mgumu, kwani hakuwa na msaada wa kupata mahitaji muhimu.

Anasema kuwa mtu pekee aliyemfanyia wema mbali na bibi yake ni daktari aliyemhudumia wakati akijifungua, akisema kwamba kamwe hawezi kumsahau.
“Sikutaka kupoteza kumbukumbu ya daktari yule, Novatus Kasongo, nikaamua kumpa jina hilo mtoto wangu, alikuwa mwema na alinisaidia,” anasema Aisha.
Msaada anaohitaji
Hatima ya familia hiyo ipo chini ya bibi Mwajabu ambaye hana shughuli nyingine anayoweza kufanya zaidi ya kilimo cha jembe la mkono. Lakini pia hawezi kulima mashamba ya mbali kwa kuwa ana jukumu la kumuangalia mjukuu wake yake huyo na kumfanyia kila kitu ikiwemo kumtoa nje na kumrudisha ndani jioni.
“Ninaishi kwa kutegemea kilimo cha jembe la mkono, lakini pia siwezi kulima sana kwa kuwa nina jukumu jingine la kumwangalia mjukuu wangu na mtoto wake,” anasema na kuongeza:
Pia siwezi kwenda mbali kwa kuwa inabidi nimwangalie mjukuu wangu, ambaye hajiwezi kwa chochote, hapa nilipo ninaumwa kifua kwa sababu ya kumbeba kila siku wakati wa kumtoa nje na kumrudisha ndani jioni,” anasema.

Anaongeza: “Ninaomba wasamaria wema wanisaidie chakula, nguo na kitukuu changu kusoma, hivi sasa umri wake anatakiwa kuwa shuleni lakini sina uwezo. ninaomba wanaoguswa na hili wanihurumie.
Pia ninaomba msaada wa kiti maalumu kwa ajili ya mjukuu wangu, akiwa na kiti itanipunguzia kazi kwani nitakuwa nikimsukuma tu.”

Habari hii ni kwa Hisani ya MPEKUZI (www.freebongo.blogspot.com)

Kindly Bookmark this Post using your favorite Bookmarking service:
Technorati Digg This Stumble Stumble Facebook Twitter
YOUR ADSENSE CODE GOES HERE

0 comments:

Post a Comment

 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |