Monday, October 28, 2013

MWANAFUNZI EDSON KUNAMBI; ISHARA YA MAFANIKIO YA ELIMU JUMUISHI TANZANIA




Mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa Mpango wa Elimu Jumuishi, utaleta manufaa na mabadiliko chanya ya kielimu kwa watoto wenye ulemavu, ikiwa utatekelezwa kama ulivyopangwa kuanzia uboreshaji wa miundombinu, vifaa, watumishi wa elimu na walimu.


Pia mkakati huo usipochakachuliwa, utaleta uaminifu zaidi kwa familia nyingi zenye watoto wenye ulemavu, hivyo kuwasukuma kuwapeleka watoto wao shuleni, kwani wataamini katika ubora wa malezi ya walimu kwa watoto hao.

Mbali na ubora wa malezi ya walimu, imani ya wazazi katika kuwapeleka watoto walemavu shuleni, itaongezeka kama shuleni kuna vifaa vya kutosha na miundombinu iliyoandaliwa kwa ajili ya kundi hilo la wanafunzi.

Kisa cha Edson Kunambi
Mazingira ya elimu yakiboreshwa na kuwa rafiki kwa walemavu, katu ulemavu hauwezi kuwa kikwazo kwa watu wenye ulemavu kushindwa kusoma. Hili limejidhihirisha kupitia kwa mtoto mwenye ulemavu wa kutokusikia na kusema, Edson Kunambi (13), mkazi wa Kibaha ambaye katika makala haya anaonyesha furaha na mafanikio anayoyapata baada ya kuchanganywa katika darasa moja na watoto wengine wasio na ulemavu
Akizungumza na gazeti hili kwa lugha ya alama, huku akitafsiriwa na mwalimu wake Idd Besha, Kunambi anayesoma darasa la tano, anasema anapenda kusoma katika shule jumuishi kwa sababu watoto wengi wako makini kujisomea, tofauti na ilivyo katika shule maalumu za watu wenye ulemavu.

Tofauti na shule aliyokuwepo awali, anasema katika darasa ya elimu jumuishi kila mtoto anajishughulisha kujifunza iwe kwa kusoma, kuchora au kufanya hesabu.
Akiwa na umri wa miaka minne, anasema alipelekwa kusoma elimu ya awali katika shule ya watoto wenye ulemavu wa uziwi Buguruni Dar es Salaam, ambako alisoma hadi darasa la tatu. Badaye akahamishiwa katika shule jumuishi anayosoma sasa ampapo mwaka huu yuko darasa la tano.

Akishirikiana vyema na wanafunzi wenzake, Kunambi amekuwa moto wa kuotea mbali darasani kwa kuwa na matokeo mazuri kushindwa wanafunzi wengi wasio na ulemavu. Kwa mfano, anasema mwaka 2012 alishika nafasi ya pili darasani.
“Mwaka huu 2013 sikufurahi sana maana nimekuwa wa 17 darasani,’’ anasema.
Mama yake mzazi, Onoratha Kunambi anasema mtoto wake huyo ni mzaliwa wa kwanza katika familia ya watoto watatu, lakini ni yeye tu mwenye ulemavu wa kutokusikia na kuzungumza.

Anaeleza kuwa Edson alizaliwa miaka 13 iliyopita kwa njia ya kawaida. Alipofikisha miezi minane na wiki mbili alianza kusumbuliwa sana na mafua. Baadaye hata alipokuwa akilia hakutoa sauti, huku mdomo ukimjaa mate mengi.
“Sisi kama wanafamilia tulianza kushtukia matatizo hayo akiwa na mwaka mmoja, lakini tukasema labda kachelewa kuongea kama inavyotokea kwa watoto wengine.Tukakaa lakini pia alikua hashtuki mlango ukijibamiza, tukaanza kuingiwa na hofu na tulipofuatilia hospitalini tukabaini alikuwa ni kiziwi pia bubu. Basi tukawa tunawasiliana naye hivyo hivyo kwa kutazamana usoni,” anasema
Mama Kunambi anakiri furaha aliyo nayo mwanawe hasa baada ya kumhamishia katika shule yenye wanafunzi wa kawaida. Kunambi naye anafurahi kuwepo shuleni hapo kwa kuwa wanafunzi wenzake wanampa ushirikiano.

Walimu wake Idd Besha na Mwamtoro Uwesu wamemwelezea Kunambi kuwa ni mpenda masomo na hapendi kucheza wakati wa vipindi, na ikitokea anamwona mwenzake anasumbua darasani haraka humfuata mwalimu na kumjulisha.
“Huyu mtoto kahamia hapa akiwa darasa na nne, tulimuweka katika darasa la wenye ulemavu lakini akaonekana tofauti sana. Tukamhamishia darasa jumuishi akawa anasoma na wenzake, na anapenda haki maana utakuta hata ikitokea mwalimu umesahihisha ukamkosesha bahati mbaya anakufata anakuonyesha na haondoki hadi umsahihishie na umuelewesha kuwa umefanya kwa bahati mbaya, hufurahi sana,” anasema mwalimu Besha.
Kwa pamoja wanasema Kunambi hupenda masomo ya Tehema, sayansi, Kiswahili na Kiingereza, huku mwenyewe akisisitiza kuwa anapenda aje kuwa mtaalamu ya masuala ya Tehama.

Kunambi ana ndoto na tayari ameshaanza kuifanyia kazi ili aitimize. Wajibu wa wadau wa elimu hasa ile jumuishi ni kuhakikisha Kunambi na wanafunzi wengi wa aina yake katika nchi hii wanajengewa mazingira wezeshi ya kutimiza ndoto zao.

http://socialworkclubtz.blogspot.com


Kindly Bookmark this Post using your favorite Bookmarking service:
Technorati Digg This Stumble Stumble Facebook Twitter
YOUR ADSENSE CODE GOES HERE

3 comments:

Unknown on April 1, 2014 at 7:29 AM said...

Hebu niambieni kuwa nyie kazi zenu mnazifanyaje kwenye jamii ya walemavu

Unknown on April 1, 2014 at 7:31 AM said...

MIMI SICOMMENT ila nataka kujua mnafanyaje kazi zenu maana nahiataji ushauri wenu

Anonymous said...

Na Mimi ni mlemavu wa kusikia ila nimehitimu elimu ya juu nikiwa na degree ya computer science, pamoja na diploma ya technolojia ya habari pia na Astashahada ya technolojia ya habari. tatizo linakuja pale tunapoitwa kwenye interview hasa ya mahojiano hapa ndipo napata wakati mgumu kwa sababu ya usikivu. naomba Serikali itoe kipaumbile kwa watu wenye disability ili nao wapate ajira. ikiwezakana walemavu wapewe kazi maalumu

Post a Comment

 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |