Mkakati
wa kitaifa wa utekelezaji wa Mpango wa Elimu Jumuishi, utaleta manufaa na
mabadiliko chanya ya kielimu kwa watoto wenye ulemavu, ikiwa utatekelezwa kama ulivyopangwa
kuanzia uboreshaji wa miundombinu, vifaa, watumishi wa elimu na walimu.
Pia
mkakati huo usipochakachuliwa, utaleta uaminifu zaidi kwa familia nyingi zenye
watoto wenye ulemavu, hivyo kuwasukuma kuwapeleka watoto wao shuleni, kwani
wataamini katika ubora wa malezi ya walimu kwa watoto hao.
Mbali
na ubora wa malezi ya walimu, imani ya wazazi katika kuwapeleka watoto walemavu
shuleni, itaongezeka kama shuleni kuna vifaa vya kutosha na miundombinu
iliyoandaliwa kwa ajili ya kundi hilo la wanafunzi.
Kisa
cha Edson Kunambi
Mazingira
ya elimu yakiboreshwa na kuwa rafiki kwa walemavu, katu ulemavu hauwezi kuwa
kikwazo kwa watu wenye ulemavu kushindwa kusoma. Hili limejidhihirisha kupitia
kwa mtoto mwenye ulemavu wa kutokusikia na kusema, Edson Kunambi (13), mkazi wa
Kibaha ambaye katika makala haya anaonyesha furaha na mafanikio anayoyapata
baada ya kuchanganywa katika darasa moja na watoto wengine wasio na ulemavu
Akizungumza
na gazeti hili kwa lugha ya alama, huku akitafsiriwa na mwalimu wake Idd Besha,
Kunambi anayesoma darasa la tano, anasema anapenda kusoma katika shule jumuishi
kwa sababu watoto wengi wako makini kujisomea, tofauti na ilivyo katika shule
maalumu za watu wenye ulemavu.
Tofauti
na shule aliyokuwepo awali, anasema katika darasa ya elimu jumuishi kila mtoto
anajishughulisha kujifunza iwe kwa kusoma, kuchora au kufanya hesabu.
Akiwa
na umri wa miaka minne, anasema alipelekwa kusoma elimu ya awali katika shule
ya watoto wenye ulemavu wa uziwi Buguruni Dar es Salaam, ambako alisoma hadi
darasa la tatu. Badaye akahamishiwa katika shule jumuishi anayosoma sasa ampapo
mwaka huu yuko darasa la tano.
Akishirikiana
vyema na wanafunzi wenzake, Kunambi amekuwa moto wa kuotea mbali darasani kwa
kuwa na matokeo mazuri kushindwa wanafunzi wengi wasio na ulemavu. Kwa mfano,
anasema mwaka 2012 alishika nafasi ya pili darasani.
“Mwaka
huu 2013 sikufurahi sana maana nimekuwa wa 17 darasani,’’ anasema.
Mama
yake mzazi, Onoratha Kunambi anasema mtoto wake huyo ni mzaliwa wa kwanza
katika familia ya watoto watatu, lakini ni yeye tu mwenye ulemavu wa
kutokusikia na kuzungumza.
Anaeleza
kuwa Edson alizaliwa miaka 13 iliyopita kwa njia ya kawaida. Alipofikisha miezi
minane na wiki mbili alianza kusumbuliwa sana na mafua. Baadaye hata alipokuwa
akilia hakutoa sauti, huku mdomo ukimjaa mate mengi.
“Sisi
kama wanafamilia tulianza kushtukia matatizo hayo akiwa na mwaka mmoja, lakini
tukasema labda kachelewa kuongea kama inavyotokea kwa watoto wengine.Tukakaa
lakini pia alikua hashtuki mlango ukijibamiza, tukaanza kuingiwa na hofu na
tulipofuatilia hospitalini tukabaini alikuwa ni kiziwi pia bubu. Basi tukawa
tunawasiliana naye hivyo hivyo kwa kutazamana usoni,” anasema
Mama
Kunambi anakiri furaha aliyo nayo mwanawe hasa baada ya kumhamishia katika
shule yenye wanafunzi wa kawaida. Kunambi naye anafurahi kuwepo shuleni hapo
kwa kuwa wanafunzi wenzake wanampa ushirikiano.
Walimu
wake Idd Besha na Mwamtoro Uwesu wamemwelezea Kunambi kuwa ni mpenda masomo na
hapendi kucheza wakati wa vipindi, na ikitokea anamwona mwenzake anasumbua
darasani haraka humfuata mwalimu na kumjulisha.
“Huyu
mtoto kahamia hapa akiwa darasa na nne, tulimuweka katika darasa la wenye
ulemavu lakini akaonekana tofauti sana. Tukamhamishia darasa jumuishi akawa
anasoma na wenzake, na anapenda haki maana utakuta hata ikitokea mwalimu
umesahihisha ukamkosesha bahati mbaya anakufata anakuonyesha na haondoki hadi
umsahihishie na umuelewesha kuwa umefanya kwa bahati mbaya, hufurahi sana,”
anasema mwalimu Besha.
Kwa
pamoja wanasema Kunambi hupenda masomo ya Tehema, sayansi, Kiswahili na
Kiingereza, huku mwenyewe akisisitiza kuwa anapenda aje kuwa mtaalamu ya
masuala ya Tehama.
Kunambi
ana ndoto na tayari ameshaanza kuifanyia kazi ili aitimize. Wajibu wa wadau wa
elimu hasa ile jumuishi ni kuhakikisha Kunambi na wanafunzi wengi wa aina yake
katika nchi hii wanajengewa mazingira wezeshi ya kutimiza ndoto zao.
http://socialworkclubtz.blogspot.com
Read More ->>