JONAS
LUBAGO
Kwa jina naitwa Jonas Lubago, natoka chama cha
wasioona Tanzania (TLB). Ninaishi Dar es
salaam ambapo nina mke mmoja na mtoto mmoja kwa sasa. Nimeajiriwa na naendeleza
shughuli zinazo husu maswala ya watu wenye ulemavu za kila siku.
Ulemavu nilionao ni ulemavu wa uoni (macho).
Historia yangu ya ulemavu siifahamu vizuri, ila kwa harakaharaka imeonekana ni
tatizo la kuzaliwa nalo ambalo limekua likiendelea kujidhihirisha kadri umri
unavoenda. Nilianza kusoma kwenye shule za kawaida na kujifunza kama watoto
wengine. Nilipofika darasa la tatu ndo walimu wakagundua kua sioni sawasawa.
Nilihamishiwa katikati ya darasa lakini sikuweza kuona, nikawekwa mbele ya
darasa lakini tatizo likabaki vilevile. Kuanzia wakati huo ndo nikaanza
kujifunza maandishi ya nukta nundu ambayo niliendelea kuyatumia katika ngazi
zote za kielimu mpaka kwenye hatua ya masters. Nina masters ya ualimu (MA
Education).
Katika maisha ndoto zinabadilika kutokana na
ngazi uliopo kwa wakati huo. Mimi sikuwaza kua nani au kushika nafasi gani,
lakini mara zote tangu nikiwa mdogo ninafikiria jinsi ninavyoweza kua kwenye
nafasi inayoweza kunipa fursa ya kuwahudumia watu wenye ulemavu na jamii kwa
ujumla. Niwe sehemu ambayo ikitokea changamoto yoyote inayo wahusu watu wenye
ulemavu na inahitaji kufanyiwa maamuzi, basi changamoto hiyo itatuliwe kwa
kutoa kauli au neno tu. Hiyo ndo nafasi ninayo tamani kuwa nayo siku moja.
Siwezi kusema nataka niwe waziri kwasababu tunaona mawaziri wengi ambao
wanashindwa kufanya maamuzi, pengine tunakosa mtu anayeweza kufanya maamuzi
ambayo athari zake zitaonekana kwenye maisha ya mtu mmojammoja.
Kwa taifa letu kuna mambo ambayo tumeishapiga
hatua, vitu kama sera, na sheria ziko nyingi sana. Kwahyo mi naona upande wa
policy work tumeisha fanya vyakutosha, lakini hizi sera na sheria zote
zinazowekwa kama hazifanyi impact kwenye maisha ya mtu mmojammoja
(individuals), bado hizi sera zinakua hazina maana sana. Ndomaana nasema
natamani niwe kwenye sehemu ambayo ntasema sera flani haijatekezwa, wewe
halimashauri flani, wizara flani, au taasisi flani fanya hiki na tukaona impact
kwa watu wenye ulemavu na maisha yao kubadilika.
Katika kuliendea swala la kupata mwenza (mke)
sikukumbana na changamoto kwakweli. Nadhani hii ilitokana na aina ya shule
nilizo zoma, mimi nimesoma intergrated schools tokea shule ya msingi. Hili
lilinipa fursa ya kuzijua skills za kukaa na watu mbalimbali tangu nikiwa
mdogo. Nilijifunza namna ya kuchangamana na kuishi na wengine, pia ni mbinu
gani unaweza kuzitumia katika kumpata mwenza. Naweza nikasema nilikua na
advantage tu, kwamba nilikua na choice nyingi za kuchangua. Tatizo linakuja kwa
jamii inayo waangalia! Watu wanaanza kujiuliza maswali, hivi huyu alimwonaje
huyu mwenzake kwamba ni mzuri? Mkienda sehemu kama kutembea watu wanawaangalia
sana, na yeye akiona hivo anaanza kujiuliza mbona watu wananiangalia sana?
Kwahiyo changamoto tulizonazo zinatoka upade wa jamii na sio upande wake yeye
au jinsi anavo nielewa au namna nilivompata.
Katika maisha kuna changamoto nyingi, zipo
zile za kitaasisi ambapo unakuta tasisi nyingi sana sio rafiki. Lakini nikivua
miwani na kujiangalia mimi mwenyewe na kuangalia jamii ya watu wenye ulemavu
naona changamoto nyingi sana.
Kuna mifumo mingi ambayo haiwafikishii
mawasiliano watu wenye ulemavu na hivyo kuwanyima haki ya taarifa. Yako
maendeleo mengi ambayo hayawalengi watu wenye ulemavu, kwahiyo wanakua nje ya
mfumo wa maendeleo yanayo ilenga jamii. Kuna uwezeshwaji ambao hauwafikii watu
wenye ulemavu. Kwahiyo ukija kuhesabu mfumo mmojammoja uliopo ndani ya jamii,
utaona kwamba watu wenye ulemavu hawajalengwa moja kwa moja. Kitu hiki
kinawafanya wawe nje ya uwanda mpana wa maendeleo ya jamii. Na ndiomaana utaona
watu wenye ulemavu wengi ni maskini, hawana elimu, wanaishi maisha ya utegemezi
na wengine wakifika sehemu watu wanawashangaa, hii ni kwasababu ya mifumo na
changamoto zilizopo.
Tukitaka kuibadili jamii yetu na kuifanya
jumuishi ni lazima tuangalie ni vitu gani ambavyo sio jumuishi kwanza.
Kwamfano, upande wa maamuzi sio jumuishi, jamii zina mitazamo ambayo sio
jumuishi. Kwahyo kwenye jamii panatakiwa pawekewe mitazamo jumuishi. Mzazi
akipata mtoto mwenye ulemavu kitu chakwanza kujiuliza itakua, mimi nimepata
mtoto ambaye ni tofauti na wengine, kwahiyo jamii itanionaje ama? Hilo nalo ni
shida. Ukja kwenye mifumo inayofuata kama elimu utagundua kua ni baguzi kabisa.
Kwasababu hauweki mazingira ya kumuingiza mtoto mwenye ulemavu kwenye mfumo
ambao unatumiwa na watoto wengine. Kwahiyo weka mfumo wa elimu ambao ni
jumuishi. Mfumo wa elimu jumuishi usichukuliwe kama
wimbo; uwe mfumo ambao mtu mwenye ulemavu wa kawaida mfano, ulemavu wa viungo,
alibino, na kadhalika ataweza kusoma kwenye shule za kawaida. Na kwa ulemavu
mwingine ambao ni mkubwa kidogo kuwe na shule kama nilizosoma mimi (intergrated
schools) shule mchanganyiko. Kwahiyo unawezakua na mifumo miwili ambayo
itaongeza nguvu kwenye swala la elimu.
Ukija kwenye mfumo wa utoaji maamuzi je
tunapata uwakilishi? Hapo ndo nafikia hatua yakusema kua hata mfumo wa uchaguzi
tunaoutumia hapa nchini, ni mfumo mbaya. Yaani yule aliyepata kura nyingi
kupita wenzake, hata kama ameongoza kwa kura moja, huyo ndo atachukuliwa kama
kiongozi wenu. Hata kama mlikua watu 100 na wakwanza akapata kura 35, hawa
waliobaki wakagawana kura chini ya 35 inamaana utakuta huyu mwenye 35 anawaongoza
watu wengine 35 ambao hawakumchagua. Sasa tungekua na mfumo wa uwiano katika
uchaguzi (propotional representation) utakao mruhusu yoyote aliyejaribu kufanya
maamuzi, hayapotei katika ngazi ya kwanza, bali yatakwenda yanakusanywa mpaka
ngazi ya taifa. Mwishowe utakuta kile alichokifanya kwenye ngazi ya chini
kabisa kinakua na athari mpaka kwenye ngazi ya taifa. Kwahiyo nasema hata mfumo
wa uchaguzi sio jumuishi na unahitajika mfumo ambao una wiano.
Nivigumu sana kuilaumu jamii kwa lolote
linalotokea kwasababu ni tamaduni ambazo tumezaliwa nazo, kinachotakiwa ni
uhamasishwaji katika nyanja zote. Kwasasahivi mabadiliko yanaonekana sio kama
zamani, zamani tulikua tunauawa baada ya
kuzaliwa, lakini kutokana na maendeleo yaliyopo na kuwafanya watu wajifungulie
hospitali inakua vigumu kuuawa tena.
Watu wenye ulemavu wanatakiwa
kujiamini, watu kama sisi ambao tumebahatika kupata elimu ndo tunatakiwa kua
vioo. Hii itaipelekea jamii kutuona na kuanza kutuamini. Kimsingi tunaacha
athari katika jamii, unapoenda sehemu na kutoa elimu kwa wazazi na jamii na
ikagundulika kua na wewe ni mlemavu inawapelekea hata wale wazazi walio waficha
watoto wao ndani kuamua kuwatoa na kuwapeleka shule.
Taasisi mbalimbali zinatakiwa zijiwekee
taratibu za namna ya kuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Kwa kiwango kikubwa naona serikali
imeishafanya mambo mengi kwa watu wenye ulemavu, kuna sera, sheria na miongozo
mbalimbali. Tatizo lililopo serikalini nikwamba hakuna mawasiliano kati ya
ngazi ya serikali kuu na halimashauri. Kama sera hizi na mipango iliyoko kwenye
ngazi ya kitaifa zingewekewa mpango wa kuwaelimisha wafanya maamuzi kwenye
ngazi ya halimashauri tungepiga hatua. Kwahiyo serikali iweke mpango
wakuwaelimisha taratibu watu wa halimashauri ili waweke maswala ya watu wenye
ulemavu katika mipango yao ya kila mwaka.
0 comments:
Post a Comment