Naitwa Abdillah Omar Abubakar, ni mweka hazina
wa chama cha Albino Tanzania (TAS) na pia ni mjumbe wa bodi ya SHIVYAWATA.
Namshukuru Mungu nimeoa na nina watoto watatu
(3). Mke wangu ni Albino vilevile ila sio kwamba nilimuoa kwasababu nisingeweza
kupata mwanamke wa aina nyingine. Ni mapenzi tu ndo yalitufanya tuoane. Vikwazo
katika jamii huwa havikosi, hususani vikwazo vya kimtizamo. Kila mzazi
anatamani mwane apate kilicho bora, huo ndo ukweli.
Nilipowambia wazazi wangu kua naoa na nikawatajia
mchumba wangu, hawakuweka shaka kua kwanini namuoa yeye? Halikadhalika wazazi
wa mwenzangu hawakuweza kuniwekea vikwazo pia. Inawezekana watu wa nje ambao
sio wazazi wetu kuanza kujiuliza maswali. Hili ni swala la kawaida tu. Lakini
baada ya kuoana tunaishi na jamii katika mazingira ambayo ni mazuri mno!
Hatukumbani na unyanyapaa wa aina yoyote. Tunashiriki kikamilifu katika
shughuli za kijamii na tunathaminiwa katika kila ngazi.
Changamoto zilizojaa katika jamii ni zile za
mitazamo. Unaweza ukafika mahala, watu kwa kukuona kwamba wewe ni Albino
wanadhani hata ule uwezo wa kufikiri huna. Mara nyingi
kupambana na changamoto hizi ni kutumia njia ya kuonesha kwa vitendo. Kwamba
pale ambapo unaona kuwa kuna kikwazo cha aina flani, basi wewe unaonesha uwezo
ili kukinzana na kile kikwazo. Kwahiyo majibu yanapotokea, ushirikishwaji na
kuaminika hupewa nafasi kubwa sana. Lakini naweza nikasema kwa
uzoefu wangu wa maswala ya watu wenye ulemavu, nimepata kuskia na kuona mambo
mengi ambapo, kama kusingekuepo na hivi vyama mimi nisingejifunza vitu vingi.
Na kwabahati nzuri ndani ya familia yangu sikuwa na unyanyapaa tokea
nilipozaliwa mpaka nakua. Kwahiyo mambo mengi nisingeweza kuyafahamu. Wazazi
wangu waliamini kuwa mimi nahitaji kua chini yao kwa maisha yangu yote. Ispokua
kutokana na kutokua na elimu nzuri ya maswala haya, kuna mazingira mengine ya
malezi walionipa mimi ambayo yalikua ni vikwanzo kwangu ila hawakujua.
Moja ya ndoto zangu kubwa ilikua ni kutoka
kwenye jamii na kufahamika, kutambulika na kusikika pia ili kutoa mchango ndani
ya jamii inayo nizunguka. Hizo ndoto zimejitokeza ambapo kwa sasa ni kiongozi
tena kiongozi wa kitaifa wa chama na vilevile kiongozi wa shirikisho ambalo
linashikilia vyama vyote vya maswala ya watu wenye ulemavu. Hivyo ndoto zangu
zimeweza kutimia kwa kiasi flani.
Moja ya ndoto zangu ilikua ni
kutokujiangalia nilivo ila nione je nina uwezo gani katika kutenda? Kwa mfano
mimi ni Albino, kwahiyo ninapozungumza sizungumzi kama albino, ila nazungumza
kama binaadamu mwenye utashi na fikra.
Maoni yangu yatajikita sana katika kauli mbiu
ya mwaka huu ‘Ondoa vikwazo ili kujenga jamii jumuishi’.
Vikwazo vilivyoainishwa hapa ni vingi, vikiwemo vile vya kisaikolojia. Kwamba
unapomwona mtu mwenye ulemavu, ukaanza kumwona kwamba si kitu utambue kua hata
yeye atajiskia kua si kitu.Hali hii inawafanya watu wenye ulemavu kujiona
kwamba wao si sahihi pale walipo. Hiki ni kikwazo cha kwanza kinachojenga
vikwazo vingi huko mbele ya safari. Vikwazo hivi humfanya mtu mwenye ulemavu
hata awapo darasani asiweze kujiona kama mtu anayeweza kusoma hivyo kushindwa
kumudu vitu vingi. Katika sehemu za mjumuiko mtu mwenye ulemavu akienda kucheza
dansi watu wakashangaa, atajiona kama kichekesho na sio mtu wa kawaida. Ile
hali ikiendelea inapelekea kudumaza akili za watu wenye ulemavu. Kwahiyo
naiomba jamii kuondoa vikwazo hivyo.
Vikwazo vingine viko katika upande wa afya;
kwa mfano kundi la albino. Hawa ulemavu wao uko katika ngozi na macho, ngozi zao hazina
uwezo wa kuhimili mionzi ya jua kutokana na ukosefu wa melanini. Sasa hawa watu
wanaathirika na jua kali, lakini elimu ya afya kwa wazazi wanao wazaa albino
kwenye mahospitali bado iko duni. Hakuna wakunga wa kutoa elimu juu ya namna ya
kuwatunza watoto wa aina hiyo. Mtoto anapofikia ule uwezo wa kuona utakuta mzazi
pasipokujua anamtuma achukue kitu flani ambacho yeye hakioni. Sasa asipo kileta
wanamchukulia kama mjeuri, hivyo hujikuta wanamfanyia harasi sana kitu mabacho
hakimpelekei mtoto kujifunza. Watu wa afya wangetoa elimu kwa jamii juu ya
albino na namna ya kuishi nao katika jamii ilikusudi nao waweze kuishi kwa
amani kama watu wengine.
Ukienda mbele katika huduma za
mashuleni, albino wanahitaji nyezo maalumu za kukuza maandishi ili waweze kuona
na kusoma kama watoto wengine. Hiki ni kikwazo kwasababu vitu hivi hakuna.
Kwamfano hata kwenye maswala ya habari za kuchapishwa kama magazeti, utakuta
mtu anaishia kusoma kichwa cha habari pekeake lakini hawezi kuendelea kusoma
maandishi mengine maana hana nyenzo za kuyakuza. Hivyo ni muhimu sana kuwa na
nyenzo za kutosha ili albino waweze kujifunza na kupata habari mbalimbali.
Mwisho; nawaomba waajiri waondoe unyanyapaa
na fikra potofu linapokuja swala la ajira kwa watu wenye ulemavu. Hii
itawapelekea watu wenye ulemavu kukuza vipato vyao na kujimudu wao na familia
zao hivyo kujenga heshima zao ndani ya jamii.
0 comments:
Post a Comment