Monday, January 7, 2013

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA KATIKA MAADIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA MAANDISHI YA BRAILLE TAREHE 4 JANUARI, 2013






HOTUBA YA MGENI RASMI


WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII


MHESHIMIWA DKT.HUSSEIN ALI MWINYI (MB)


KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA
MAANDISHI YA BRAILLE TAREHE 4 JANUARI, 2013

·        M/kiti wa Taasisi ya Huduma na Maendeleo kwa Wasioona Tanzania
·        Ndugu Viongozi, Wadau na Wanachama wa Taasisi ya Huduma na Maendeleo kwa Wasioona,
·        Wananchi wote mliohudhuria hapa, Mabibi na Mabwana.

Kwanza kabisa napenda kuwatakia heri ya mwaka mpya 2013. Pili napenda nichukue fursa hii kuwashukuru kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii muhimu sana katika kuenzi mchango wa mgunduzi wa maandishi ya Braille ambayo yameleta ukombozi mkubwa wa maisha ya wasioona ulimwenguni kote. Wizara yangu inapenda kuipongeza Taasisi ya Huduma na Maendeleo kwa Wasioona Tanzania (TNIB) pamoja na wadau wote wa masuala ya watu wasioona kwa kuamua kuiadhimisha siku hii hapa Tanzania kwa mara ya pili.
Nafahamu kuwa Mataifa mengine Duniani yamekuwa yakiadhimisha siku hii miaka mingi iliyopita, hata hivyo wahenga husema kuwa kawia ufike, hivyo na sisi tumekwishaungana na Mataifa hayo na tutaendelea kuienzi siku hii muhimu.

Ndugu Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kulipongeza Kanisa la Anglikan Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuanzisha shule kwa ajili ya Wasioona. Aidha nayapongeza madhehebu mengine pamoja na Serikali kwa kufuata mfano huo, jambo ambalo limesaidia sana kubadili mtizamo hasi na potofu dhidi ya watu wasioona kuonekana kwamba hawana mchango wowote katika maendeleo ya Taifa na Jamii zao. Wasioona ni nguvu kazi ambayo haina budi kuendelezwa kwa faida yao na Taifa kwa ujumla. Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na kutoa msaada kwa Asasi mbalimbali zinazojihusisha na uboreshaji wa maisha ya watu wasioona nchini. Hii inathibitishwa na hatua ya Serikali ya kutengeneza Sera na Sheria maalum ya watu wenye ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010. Hatua hii itasaidia sana kuhakikisha kwamba haki za msingi za wasioona na watu wenye ulemavu kwa ujumla zinalindwa na kutekelezwa.
Serikali imeishatunga Kanuni za Sheria hiyo, hivyo ni kazi ya Serikali na Asasi zote za watu wenye ulemavu kuwaelimisha wadau wao kuifahamu sheria hii na kudai haki zao kisheria.

Ndugu Mwenyekiti, napenda niwapongeze sana Wasioona wote kwa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali na Asasi za Kiraia katika kujiendeleza Kielimu na  Kiuchumi. Wasioona wengi wanavyo vipaji na uwezo katika nyanja mbalimbali ambavyo vikitumika vizuri Taifa linaweza kunufaika kwa vipaji vyao. Kwa kutumia sheria ya Watu wenye Ulemavu, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali itaweka mikakati endelevu itakayowezesha watu wenye ulemavu kufurahia maisha yao kama raia wengine. Pia napenda niwahakikishie kuwa Baraza la watu wenye ulemavu litaundwa haraka iwezekanavyo pamoja na kuzindua mfuko maalum wa watu wenye ulemavu ambao utasaidia sana kuwezesha shughuli zenu kuendeshwa kwa uhakika.

Ndugu Mwenyekiti, nafahamu kua mko katika mchakato wa kuanzisha mradi wa Kiwanda kidogo cha kutengeneza fimbo nyeupe zinazotumiwa na Wasioona. Serikali kupitia Wizara yangu iko tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha kwamba mradi huu unafanikiwa. Fimbo nyeupe imetambuliwa rasmi kisheria katika Sheria ya watu wenye Ulemavu, hivyo ni wajibu wa Wizara yangu kuona kwamba mpango huu unafanikiwa. Kwa kuunga mkono jitihada zenu napenda kutoa changamoto kwa watu binafsi, mashirika na Serikali kwa ujumla kuona umuhimu wa kuchangia mradi huu. 

Ndugu Mwenyekiti, kuhusu changamoto zinazowakabili katika upatikanaji wa vifaa na machapisho mbalimbali katika Breille, Wizara yangu itashirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tamisemi kuzipunguza changamoto hizi. Ninawaomba wasioona wote hususani wenye umri wa kwenda shule wapelekwe shuleni na wale ambao umri wa kwenda shule umepita wapelekwe katika vyuo mbalimbali vya mafunzo ili kuwapatia stadi na ujuzi wa kuwawezesha kujitegemea. Pia napenda kutoa wito kwa wananchi wote kuhakikisha kwamba wanatunza Afya ya macho yao na wanapoona kuwa wanasumbuliwa na matatizo ya macho wasisite kwenda katika Hospitali zilizo karibu nao. Kwakufanya hivyo wataweza kubaini haraka na kuepusha athari zinazoweza kuwasababishia kutoona.

Ndugu Mwenyekiti, mwisho napenda niwapongeze sana kwa kuandaa maadhimisho haya na pia niwashukuru wadau mbalimbali waliochangia kwa hali na mali kufanikisha maadhimisho haya. Naahidi kuwa kuanzia maadhimisho yajayo Wizara yangu itaendelea kuchangia katika kufanikisha maadhimisho haya.
Napenda  niwashukuru tena kwa kunialika kuwa Mgeni rasmi katika maadhimisho ya mwaka huu. Nawatakieni mafanikio mema katika shughuli zenu na heri ya mwaka mpya 2013.

Asanteni sana kwa kuniskiliza.

Kindly Bookmark this Post using your favorite Bookmarking service:
Technorati Digg This Stumble Stumble Facebook Twitter
YOUR ADSENSE CODE GOES HERE

0 comments:

Post a Comment

 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |