Monday, January 21, 2013

MASAHIBU YA BINTI STAMILI





Ilikuwa asubuhi moja ya mwezi wa nane mwaka jana 2012 pale mimi na mwenzangu dada Mossi Magere tulipofika katika kijiji cha Ugute, kata ya Isalavanu, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kufanya utafiti. Kazi hii tulitumwa na Kituo cha Habari kuhusu Ulemavu (Information Centre on Disability-ICD) cha jijini Dar es salaam.Lengo lilikuwa kuchunguza masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa haki za watu wenye ulemavu nchini mwetu.
Mwenyeji wetu alikuwa na wazo jingine kabla hajatukutanisha na familia zenye watu wenye ulemavu. Akatuomba tuongozane naye kwenda kumjulia hali binti mmoja. Nje ya nyumba ile ya udongo mlango ulikuwa umefungwa kwa nje na kufuli, mwenyeji wetu akachepuka kidogo pembeni na kuinua kitu fulani na kutoa ufunguo.Akafungua mlango na kutuambia tuingie ndani. Mpaka wakati huo japo nilikuwa najua tuko pale kufanya nini, lakini namna mambo yalivyokuwa yanaenda ikanipa mshangao kidogo.
Tukaingia ndani. Katikati ya chumba kikubwa kulikuwa na kitu kama kilichofunikwa na matandiko. Stamili! Stamili! Mwenyeji wetu akawa anaita huku akitikisa na kujaribu kufunua matandiko yale. Ndipo nikajua kuwa aliyelala pale ni binti tuliyekuja kumwona. Hali iliyokuwa mle hakika iliniliza mimi na mwenzangu dada Mossi Magere.
Pale chini kwenye sakafu ya udongo alikuwa amelala binti Stamili, mwenye ulemavu wa viungo. Kila mwenyeji wetu alipojaribu kumwongelesha alikataa na kujaribu kujifunika zaidi na matandiko yake. Hakika matandiko yale yalikuwa katika hali mbaya kutokana na kujaa mkojo na uchafu mwingine. Kwa habari tulizozipata pale binti yule anafungiwa ndani na mama yake mzazi kila siku atokapo kwenda shambani au katika shughuli zingine za nje.
Binti Stamili alikuwa katika hali dhoofu akikabiliana na upweke mkubwa wa kufungiwa ndani masaa 24 huku akiachwa kujisaidia pale pale. Matandiko yalikuwa yamejaa mkojo na uchafu mzito, dhahiri ikionesha hakuna huduma yoyote anayopata ili kumweka katika hali nzuri. Nyumba ile ilikuwa ikivuja na kupitisha ubaridi mkali wote ukimwelekea binti yule mwenye ulemavu.Cha kushangaza mama yake mzazi halali katika nyumba ile bali anayo yake pembeni ambayo ina hali nzuri ukilinganisha na ya Stamili. Tukabaki tunajiuliza maswali mengi ambayo yalikosa majibu maana mama yake hatukubatika kumpata kwani alikuwa shambani.
Baadae alikuja dada yake ambaye naye anaishi katika nyumba nyingine na tukamuuliza maswali kadhaa. Dada yule ilibidi kumbana sana mpaka kuweza kueleza machache. Kwamba hapo awali Stamili alikuwa anaruhusiwa kutoka nje na kutembea huku na kule katika mazingira jirani na nyumbani ni hali ambayo ilitulazimu kuuliza maswali mengi yaliyokosa majibu ya uhakika. Dada yake akasema pia kwamba mama yake mzazi huenda anamfungia ndani kwa hofu kwamba asije kubakwa. Lakini hiyo sababu haikuweza kuturidhisha. Mbona sasa binti huyu amejaa uchafu utadhani si binadamu aliyeko pale! Tukazidi kujiuliza.
Kwa ufupi ni kwamba Stamili ametelekezwa na familia yake, ndugu, jamaa, marafiki na serikali hasa mamlaka ya serikali za mitaa, ikiwa ni pamoja na uongozi wa kijiji na kata. Kwa upande wa Halmashauri ya Mufindi viongozi pale walisema kwamba hawana taarifa kuhusu masahibu ya binti yule. Tulichofanya sisi kama watafiti tulihakikisha tumeacha taarifa kwa afisa ustawi wa jamii pamoja na ofisi ya elimu (msingi). Vilevile mratibu wa masuala ya walemavu katika kata ya Isalavanu bwana Emilio Mbata tulimsihi sana afikishe kilio chetu kwa wadau wote ili waweze kumsaidia binti Stamili.
Hivi majuzi tarehe 17.1.2013 nikiwa Mufindi kwa mara nyingine tukitengeneza documentary film (filamu makala?) niliweza kufika katika kijiji cha Ugute tena.Kwa mshangao wangu hali ya binti yule bado ni mbaya na mwili wake unatisha.Sasa hivi wadudu mwilini na harufu kali chumbani mle ni hali ambayo hutapenda kukutana nayo. Bila shaka Stamili kama wasichana wengine atakuwa anapata siku zake za mwezi, lakini ni msichana ambaye hayajui maji, ni hali ngumu kuifikiria. Mama yake hatukuweza tena kumpata angalau tusikie machache toka kwake.
Kwa ufupi ni kwamba baada ya kurudi Mafinga (Makao makuu ya wilaya ya Mufindi kutoka kijijini Ugute ili kuendelea na shughuli nyingine, tulikutana na Afisa Ustawi wa Jamii (sio yule wa mwanzo) na kumweleza habari hii. Alichoahidi ni kwamba atachukua hatua. Kwa makala hii naomba kumsihi Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mufindi ndugu Shimwela Limbakisye achukue hatua madhubuti kuingilia kati ili binti yule aweze kupata matibabu sahihi (rehabilitation) na kurudishiwa utu wake. Naandika hivi nikiamini kaka Shimwela atafanya hivi maana baadhi  ya watu wenye ulemavu pale Mafinga wamemtaja kama mtu anayejali sana. Ushahidi wa video wa hali ya binti huyu upo kama ikihitajika utolewe kuthibitisha haya kwa hatua zaidi za kumsaidia.
Hali kama hii ya binti Stamili ni hali halisi ya watu wengi wenye ulemavu nchini Tanzania. Iko hivyo wakati Tanzania ikiwa tayari ilisharidhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu wa mwaka 2006 (The United Nations Convention on Persons with Disabilities of 2006) na ikapitisha sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 (Persons with Disabilities Act of 2010) ya Tanzania Bara.
Masahibu yanayomkuta binti Stamili mwenye ulemavu wa viungo ni miongoni mwa changamoto nyingi sana dhidi ya watu wenye ulemavu mbalimbali duniani ambazo zilisababisha Umoja wa Mataifa kuandika Mkataba wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu wa mwaka 2006.Mkataba huu ni chombo cha kisheria cha kimataifa ambacho kinazibana nchi zilizoridhia kuhakikisha kwamba haki za watu wenye ulemavu zinalindwa. Mkataba huu ni hatua kubwa ya kubadili mitazamo hasi katika jamii zetu kuhusu ulemavu na kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata nafasi ya kufurahia siku za maisha yao sawa na watu wengine.
Mkataba huu unalenga kuendeleza, kulinda na kuhakikisha watu wenye ulemavu wanafurahia haki zao za kibinadamu. Haki hizo ni kama vile kupata elimu, huduma za afya, ajira, kupata habari na uhuru wa kufanya mawasiliano , urahisi wa kwenda mahali kokote kama vile katika majengo na kupanda vyombo vya usafiri kwa urahisi, kushiriki katika siasa, kuheshimiwa nakadhalika.
Nchi yetu iliridhia mkataba huu mwaka 2009 na kulazimika kuanza kuchukua hatua za kuutekeleza ambapo mwaka 2010 ilipitishwa sheria ya watu wenye ulemavu. Sheria hii inaielekeza serikali na vyombo mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanafurahia maisha kwa kupata huduma za afya, elimu, ajira, na kushiriki katika kila jambo ndani ya jamii yetu bila kunyanyapaliwa au kusahauliwa kwa namna yoyote ile.
Tukitazama mfano wa binti Stamili, huyu ana wakati mgumu sana kwa sababu anakabiliana na unyanyapaa kuanzia ndani ya familia yake.Watu wanaomzunguka kuanzia mama yake mzazi, na ndugu wengine hawana muda naye na anakosa haki zake nyingi tu. Anafungiwa ndani masaa 24, na anaachwa alale kwenye sakafu yenye baridi kali. Afya yake inazifi kudhoofika siku hadi siku na bila shaka hata athari nyingine za kisaikolojia zinazidi kumsonga. Si kiongozi wa serikali ya kijiji, kata, wala halmashauri ya Mufindi aliye tayari kuchukua hatua kutekeleza matakwa ya sheria ya watu wenye ulemavu ambayo ilitungwa kuwalinda watu kama Stamili licha ya kuwa taarifa kumhusu zimetolewa mara kadhaa kwa mamlaka hizo.
Halmashauri/manispaa za wilaya zinatajwa na sheria hii kama wadau wakubwa wa kulinda haki za watu wenye ulemavu. Lakini jambo moja ambalo lililojitokeza katika utafiti wa ICD ni kwamba sheria hii ya kulinda haki za watu wenye ulemavu haifahamiki kabisa na maofisa wengi wa halmashauri na manispaa. Hata utafiti uliofanywa hivi karibuni na Foundation for Civil Society umeonesha udhaifu huo mkubwa katika kutetea haki za watu wenye ulemavu. Hata maofisa wa ustawi wa jamii nchini ambao pia wanatajwa na sheria hii kama chombo kikubwa cha kulinda haki za watu wenye ulemavu bado wengi hawaijui huku utendaji wao wa kazi ukikabiliwa na mapungufu mengi hasa ya kibajeti.
Ili binti Stamili na watu wengine wenye ulemavu nchini mwetu waweze kuishi kwa furaha kama watu wengine ni lazima Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Sheria ya Watu wenye Ulemavu vitekelezwe angalau kwa viwango fulani vinavyotia moyo. Sheria inataka kuwepo mfuko wa kitaifa wa watu wenye ulemavu, basi uundwe. Sheria inataka kuwepo na daftari la watu wenye ulemavu wote nchini, lianzishwe orodha yao ijulikane na pale walipo ili iwe rahisi kushughulikia mambo yao.
Halmashauri za wilaya na manispaa zote nchini zitenge fedha maalumu za kushughulikia huduma kwa watu wenye ulemavu.Mipango yao ya maendeleo ijumuishe pia masuala yanayohusu watu wenye ulemavu (mainstreaming). Namna hiyo itakuwa rahisi hata pale taarifa za watu kama Stamili zikifika halmashauri zikafanyiwa kazi kirahisi kwa kuwa maofisa watajua kuwa fedha zipo.
Sina hakika Tanzania imefikia wapi na utekeleza wa mambo yaliyoainishwa katika Mkataba wa Kimataifa wa Watu wenye Ulemavu. Labda kama tukiweza kusoma taarifa ya utekelezaji inayotakiwa kutumwa Umoja wa Mataifa tutajua. Lakini vyovyote vile ilivyo hali bado ni mbaya sana kwa watu wenye ulemavu. Unyanyapaa bado upo mwingi tu. Shule wanakosoma watoto wenye ulemavu, ziwe zile jumuishi au zile maalumu, bado zinakabiliwa na mapungufu mengi ya vifaa vya kusaidia utoaji na upataji elimu. Mawazo hasi kwamba ulemavu ni janga au nuksi katika familia bado yapo katika jumuiya zetu na yanasababisha watu wenye ulemavu kunyanyapaliwa katika kila kona ya maisha yao. Waajiri nao wanatakiwa kisheria kutoa ajira kwa watu wenye ulemavu angalau kwa kiwango fulani (kimetajwa katika sheria), lakini bado kusitasita ni kwingi mno.
Njiani kutoka kijijini Ugute, kata ya Isalavanu, wilaya ya Mufindi, kurudi Dar es salaam, naambiwa binti Stamili bado yupo ila sina hakika lini ataweza kuonja matunda ya uhuru unaotajwa katika sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010. Natumaini Mufindi imenisoma.
Moses Gasana
Mawazo Chanya Media
0713480670
mosesgasana@yahoo.com







Kindly Bookmark this Post using your favorite Bookmarking service:
Technorati Digg This Stumble Stumble Facebook Twitter
YOUR ADSENSE CODE GOES HERE

0 comments:

Post a Comment

 

| DISABILITY IN TANZANIA INFORMATION PLATFORM © 2012. All Rights Reserved |Designed by MIRAMBO GROUP | Back To Top |