Naitwa Oram Cliphord Makaranga, ni mwenyekiti
wa chama cha albino wilaya ya Bunda. Nina ulemavu wa ngozi (albino) nilizaliwa
hivi kwa mapenzi ya Mungu. Maisha yetu ni mabaya sana kwakweli maana
hatuvumilii kukaa kwenye jua kabisa.
Jua limeisha nichomaa mpaka mwili wangu
unazeeka sasa. Lakini namshukuru mkuu wa wilaya ya Bunda na mkuu wa mkoa wa
Mara kwani wanatusimamia na kututetea na kutusaidia ingawaje sio viongozi wote
wanaofanya hivo.
Changamoto yangu kubwa ni swala la afya, tunaumwa
kwakweli. Kwamfano mimi ninasumbuliwa na saratani ya ngozi, namshukuru mkuu wa
wilaya ya Bunda na mkuu wa mkoa wa Mara kwa kuweza kunisaidia na kunipa usafiri
wa kunipeleka kwenye matibabu katika hospitali za Muhimbili na Ocean Road Dar
es salaam. Lakini pamoja na hayo, mazingira tunayo ishi ni mabaya sana
kwakweli, hatuna nyenzo za kutuwezesha kukaa kwenye kivuli muda wote.
Tunaiomba serikali ituthamini pamoja na
kutupa misaada ya kila aina ili na sisi tujiskie kwamba hii nchi ni yetu na
tunaishi salama. Wakati matamasha mbalimbali yanafanyika, kwa mfano siku ya
walemavu kitaifa sisi hatuhusishwi kabisa, serikali inatutenga kabisa, wanakua
kama hawatujui wala kututhamini. Hata kulala tunalala kwa shida, kusafiri kwa
shida, kula kwa shida na tunataka tufike kwenye tamasha letu nasisi kama
walemavu lakini kwakweli hawatuthamini. Nawaomba viongozi walioko madarakani
watuthamini kama watu wengine.
Kinacho nisikitisha nikuona wazazi waliotuzaa
wanatufukuza nyumbani nakutwambia twende kujitegemea. Tunaomba wazazi wetu
watuthamini na kutupenda kama watu wa kawaida. Nilipopatwa na matatizo ya kansa
nilichangiwa na marafiki zangu fedha za kunisaidia lakini wazazi wangu
hawakunisaidia kabisa. Namwomba Mwenyezi Mungu awasaidie wawe na mapenzi na
sisi, kwa mfano mimi nathaminiwa sana na watu wa nje kuliko wazazi wangu.
0 comments:
Post a Comment